Kuuliza Maswali Bora
Utangulizi
Kama watangazaji na watayarishaji, tunauliza maswali mengi kila siku. Kutengeneza miongozo yetu ya utangazaji, programu zetu na ripoti zetu inategemeana na namna tunavyopata taarifa. Kwa kawaida tunauliza maswali haya katika muktadha wa mahojiano (pata maelezo zaidi kuhusu jinsi ya kuunda na kufanya mahojiano yenye mafanikio hapa). Mara nyingi, kwa haraka kupata habari tunayotaka, au kwa sababu tuna mawazo ya awali ya kile tunachotaka au tunatarajia mhojiwa wetu kusema, tunauliza kile kinachoitwa "maswali ya kuongoza." Haya ni maswali ambayo yanaweza kufanya iwe vigumu kwa mhojiwa kujibu kwa uwazi na uaminifu kwa sababu yanamtaka mhojiwa kujibu kwa njia fulani. Ili kuwaheshimu wahojiwa wako na wasikilizaji wako, ni muhimu kuuliza maswali bora zaidi, ambayo hayamfanyi mhojiwa kutoa jibu kwa sababu tu anaamini anayehoji anatarajia kusikia hivyo.
Tunamaanisha nini tunaposema "maswali bora?"
Maswali bora ni maswali ambayo hayaegemei upande wowote, hayana upendeleo na yana uwazi. Yanawasaidia wahojiwa kusimulia hadithi zao kwa kutoa habari za wazi, kwa maneno yao wenyewe bila kushawishiwa na anayehoji.
Maswali bora yanaondoa maswali yenye kutoa mwongozo. Maswali ya kuongoza yanatoa mwelekeo kwa mhojiwa kuhusu jinsi wanavyotarajiwa kujibu. "Humwongoza" mhojiwa kwa kile anayehoji anataka au anatarajia kusikia.
Maswali bora hupokea majibu bora – kwa uwazi zaidi, uaminifu, na kwa namna ya kushangaza.
Kuuliza maswali bora kunawezaje kunisaidia kuwahudumia wasikilizaji wangu vyema zaidi?
• Kuuliza maswali bora huongeza nafasi ambayo wahojiwa watatoa, na wasikilizaji watasikia, majibu yenye manufaa—majibu ambayo yana maelezo ya kutosha juu ya mada.
• Inapunguza uwezekano wa wahojiwa kukwepa mada ambayo wangependelea kuepuka.
• Husaidia kuhakikisha kwamba wasikilizaji wanaweza kuelewa vyema kile mhojiwa anachoamini na kuhisi.
• Husaidia kudumisha kipengele cha mshangao katika mahojiano, na kufanya mahojiano kuvutia zaidi kusikiliza. Maswali yanayoongoza yanahimiza majibu mahususi.
• Kupitia maswali ya ufuatiliaji, inaweza kuongeza kiasi cha maelezo katika majibu.
• Ni aminifu zaidi na kwa hivyo ni halali zaidi kiuandishi wa habari.
Je, kuuliza maswali bora kunawezaje kunisaidia kuzalisha programu bora zaidi?
• Kujifunza nidhamu ya kuuliza maswali bora huruhusu udadisi, msingi wa uandishi bora wa habari, kuwa nguvu ya kuendesha kila mahojiano.
• Ni aminifu zaidi kwani huondoa imani na matarajio ya mwandishi wa habari kutoka kwenye maswali.
• Inazuia kuonekana hali ya upendeleo katika programu.
• Inamsaidia mwandishi wa habari kuelewa hadithi ni nini, na sio kile walichofikiria kuwa hadithi.
Je, nitaanzaje? (Pata maelezo zaidi kuhusu haya na mambo mengine katika sehemu ya Maelezo hapa chini.)
1. Panga mahojiano yako.
2. Jihadhari na aina mbalimbali za maswali na madhumuni yake.
3. Andika maswali yako, epuka maswali ya kuongoza.
4. Andaa maswali ambayo ni mahususi, kulingana na utafiti wako.
5. Tayarisha aina mbalimbali za maswali.
6. Kuwa tayari kuuliza maswali mazuri ya kufuatilia
Maelezo
1. Panga mahojiano yako.
Ni muhimu kupanga mahojiano yako daima. Kwanza, bila shaka, unahitaji kupata mtu sahihi wa kushughulikia suala au uzoefu unaochunguza. Mtu huyo anapaswa kuwa na ujuzi na uzoefu muhimu. Mara tu unapomchagua mtu anayefaa, amua ni nini unataka kujifunza kutoka kwake. Kujua hasa unachotaka kujua ni muhimu katika kuunda maswali bora.
Pia ni muhimu kufanya utafiti wako juu ya mada. Kadiri unavyojua zaidi kuhusu mada hiyo na mhojiwa, ndivyo maswali yako yatakavyokuwa bora zaidi.
Neema ni mkulima mdogo na mumewe Godfrey na watoto wao wawili. Wanaishi kwenye ardhi ya hekta moja na nusu katika eneo kame la Dodoma nchini Tanzania. Wanalima mahindi, pamoja na mihogo na viazi vitamu. Familia imeweza kujilisha na kupata kiasi kidogo cha pesa. Lakini afisa ugani aliwaambia kwamba wanapoteza sana kile wanachokuza. Alimwambia Neema kuwa kiasi cha asilimia 20 ya mahindi yake hupotea kila mwaka kutokana na mbinu mbaya za uvunaji na uhifadhi usiofaa. Uharibifu wa wadudu ni wa mara kwa mara na wa gharama kubwa. Amependekeza kuwa pamoja na wakulima wa jirani, Neema na Godfrey wajifunze zaidi mbinu bora za uvunaji na uhifadhi. Neema anataka lakini mumewe anahofia mbinu mpya, akipendelea kulima kama shamba la majirani zao. Anahofia kuhusu suala la kudhihakiwa.
Katika hali hii, mahojiano na Neema yangechunguza mbinu zake za sasa za kuvuna na kuhifadhi na kujua ni kwa nini mumewe, kama wengine wengi katika eneo lake, anasitasita kujaribu mbinu mpya. Hili linaweza kuwa mada nyeti kwa sababu katika nyumba ya Neema, mume wake kwa kawaida yeye ndiye hufanya maamuzi. Kujaribu kumshawishi abadili jinsi wanavyolima kunaweza kumaanisha kubadili jinsi maamuzi yanavyofanywa. Katika hali kama hii, ni muhimu kuhakikisha Neema anajua kwamba maswali yanaweza kwenda zaidi ya kilimo na kugusa jinsi wanavyofanya maamuzi ya kilimo, na kuhakikisha Neema yuko tayari kujibu maswali haya. Mpango ungekuwa kumtembelea katika shamba lake na kufanya mahojiano nnje karibu na magunia ya mahindi ya mavuno ya hivi majuzi. Mahojiano hayo yangeanza kwa maelezo ya mahali alipo, jinsi zao la mwaka huu lilivyofanikiwa, jinsi yeye na Godfrey walivyovuna mahindi, jinsi wanavyoyahifadhi, na iwapo wangefikiria kubadilisha mbinu zao ili kupunguza hasara. Katika hatua hii, unaweza kuuliza maswali kuhusu mienendo ya familia. Unajua kutokana na kuzungumza na afisa ugani katika utafiti wako kwamba wakulima hawa wawili wanaweza kutarajia kupoteza asilimia kubwa ya mahindi katika uvunaji, uhifadhi na usafirishaji wa mahindi, na hivyo basi, kupoteza pia kiasi kikubwa cha fedha.
2. Jihadhari na aina mbalimbali za maswali na madhumuni yake.
Moja ya vizuizi vikubwa vya kuuliza maswali bora ni swali linaloongoza.
Maswali yanayoongoza yanaweza kukufikisha kwenye hoja yako haraka kwa sababu unamwongoza mhojiwa kulifikia. Lakini hilo ndilo tatizo. Ni hoja yako unawapelekea. Sio yao.
Ufafanuzi wa swali la kuongoza: Swali linaloongoza ni swali linalohimiza jibu fulani, mara nyingi jibu ambalo linatarajiwa au linalotarajiwa na anayehoji. Maswali yanayoongoza mara nyingi huongoza kwa sababu ya jinsi swali linavyowekwa. Wakati mwingine, maswali yanayoongoza yanaweza kujumuisha jibu linalohitajika katika vifungu vyao wenyewe. Kwa mfano,
Neema naona umevuna mahindi yako lakini inaonekana ulikuwa na mwaka duni. Je, hapakuwa na mvua ya kutosha?
Kwa kweli Neema alikuwa na mwaka mzuri sana. Ana nafasi ndogo tu ya kupanda mahindi. Lakini swali linafanya iwe vigumu kwake kueleza hilo. Anayehoji kwanza anatoa kauli na Neema anaweza kuona ni ufedhuli kuipinga. Swali halisi halikuwa kuhusu mavuno bali ni mvua. Swali bora litakuwa:
Neema, mavuno yako ya mahindi yalikuwaje mwaka huu?
Neema anaweza kujibu hilo kwa urahisi. Mavuno yake yalikuwa juu ya wastani. Wakati mahojiano yanafanyika kando ya magunia ya mahindi, Neema anaweza hata kuyaangalia na kuelezea mavuno yake. Maelezo ya sauti yanaweza kuunda picha thabiti za kuona kwa msikilizaji.
Swali la kufuatilia juu ya mavuno linaweza kuwa:
Ni mambo gani yaliyoathiri mavuno?
Neema anajua vizuri zaidi kuliko anayehoji ni kiasi gani cha mvua ilinyesha na kama kulikuwa na sababu nyingine za kuwa na mavuno mazuri. Anaweza kuzungumza kwa kirefu kuhusu uzoefu wake mwenyewe bila kuhisi kama anahitaji kuzingatia swala la hali ya hewa. Asili ya wazi ya "Mambo gani ...?" humpa Neema uhuru wa kuzungumza kuhusu masuala muhimu yanayomkabili. Maswali ya kufuatilia yatatokana na jinsi atakavyojibu.
Njia nyingine ya kuelewa maswali yanayoongoza ni kusema kwamba yanaongoza kwa sababu ya Maswali yenya muongozo, maswali ya udadisi yenye muongozo, au maswali ya hisia.
Maswali ya muongozo. Haya ni maswali ambayo humfanya mhojiwa kuwajibika zaidi au kupendelea kutoa jibu fulani, hasa ikiwa jibu hilo linatazamwa na mtu anayehojiwa kama linalohitajika.
Neema, unatumia mbegu bora za mahindi?
Swali linaonekana kutokuwa na upande na halitoi muongozo mwanzoni. Lakini linaweza kuwa swali la mwongozo, au kuweka njia nyingine, kumsukuma Neema kusema ndiyo kwa sababu anafikiri kwamba kutumia aina zilizoboreshwa kunachukuliwa kuwa jambo zuri—au ni jambo ambalo adhma ya anayehoji anaona kutumia mbegu bora ndio inafaa. Ni muhimu kukumbuka kwamba, kwa ujumla, wahojiwa huwa wanataka kutoa majibu ambayo yanampendeza yule anayehoji, na majibu ambayo yanajionyesha kuwa ni mazuri. Swali bora la kuuliza ni:
Neema unatumia mbegu za aina gani?
Kwa hivyo, ili kuepuka kuuliza maswali yenye muongozo, kuwa mwangalifu kuuliza maswali ambayo a) hayana maneno yanayopendekeza jibu linalohitajika, na b) ni ya jumla iwezekanavyo huku ukiendelea kupata taarifa unayohitaji.
Hapa kuna mfano mwingine wa swali la muongozo, na swali mbadala ambalo ni bora.
Je, unapendelea kutumia mbinu mpya na bora za uvunaji ili kupunguza upotevu wa mazao ambayo baadhi ya wakulima katika eneo hili hutumia?
Maneno "unapendelea" na "ufanisi" yanamuelekeza Neema kwenye jibu linalohitajika, iwe anapendelea mbinu hizo au la. Badili swali hilo na maswali haya yasiyo na msingi ambayo yanamruhusu kujibu kwa uaminifu zaidi.
Je, huwa unaweza kujua kama umepata hasara ya mazao, kabla au baada ya kuvuna?
Unadhani sababu zake ni zipi?
Unahisi nini kuhusu mbinu mbalimbali za uvunaji ambazo baadhi ya wakulima wanajaribu?
Kwa kuepuka maswali ya kuongoza, unaweza kuishia kuuliza maswali zaidi, lakini ni maswali ambayo Neema anaweza kujibu kutokana na uzoefu wake wa maisha. Yeye ndiye mtaalam hapa, sio anayehoji. Maswali ya wazi yanampa fursa ya kushiriki ujuzi wake.
Matumizi ya neno "kutokea" katika swali hilo la kwanza ni chaguo la kuvutia. Watafiti wanapendekeza kwamba kutumia neno hilo, kama vile “Je! unajua…” ina maana kwamba Neema hatarajiwi kutoa jibu chanya. Kutotumia neno "tokea" huondoa matarajio hayo, na kumwacha Neema huru kuzungumza kutokana na uzoefu wake.
Vidadisi vyenye kuongoza: Vidadisi hutumika kuchimba kwa undani kidogo jibu au taarifa ya mhojiwa. Maswali haya ya udadisi ni muhimu sana na yanafaa katika mahojiano, lakini maswali dadisi yenye kuongoza hayafai. Kwa hila (au si kwa hila) huelekeza mhojiwa kujibu kwa njia fulani, kwa kifupi ni kwamba "kuweka maneno kinywani mwa mhojiwa." Kwa mfano, hapa kuna swali la udadisi kwa Neema.
"Je, unasema kwamba aina mpya za kuhifadhi zilizowasilishwa na afisa ugani hazifanyi kazi?"
Neema alimwambia anayehoji kuwa kuhifadhi mahindi yake kwenye mifuko, jinsi ambavyo amekuwa akifanya siku zote, ilikuwa bora kwake na kwa Godfrey. Anayeongoza mahojiano aliuliza tena swali la udadisi ili Neema afafanue kile alichokua anamaanisha. Swali la udadisi linamfanya anayehojiwa kufikiria zaidi na kupata wazo ambalo hapo awali halikuwepo kwenye kichwa chake. Ni la kichokozi pia kwani humfanya Neema pia asiwe huru zaidi na kujiona kwamba ni mwerevu zaidi kuliko mtaalamu wa ugani.
Badala yake, swali la udadisi linapaswa kuwa wazi, kwa mfano:
Unamaanisha nini kusema hivyo? Au - Unaweza kuelezea tafadhali?
Maswali yenye kubeba hisia: Swali la kuonyesha hisia ni swali lenye kuonyesha kwamba ukweli fulani ni kweli, ingawa ukweli wake haujathibitishwa. Kujibu swali la aina hii kunamweka mhojiwa katika hali ya mtanziko. Chukua kwa mfano swali hili alilomuuliza Neema:
Unadhani afisa ugani alikuwa anadanganya alipokuambia unapoteza asilimia 20 ya mazao yako?
Neno "uongo" ni neno lenye nguvu sana. Linabeba swali kwa kupendekeza kwa uwazi kwamba afisa ugani, kwa kweli, ni mwongo. Ni swali lisilo la haki kumuuliza Neema, kwani asingejua nia ya mtu huyo. Inaweza kusababisha jibu lisilo la kweli au la upendeleo. Pia si haki kwa afisa ugani.
Njia bora ya kuuliza swali hilo ni hii:
Una maoni gani kuhusu taarifa ya afisa ugani kwamba unapoteza 20% ya mahindi yako kabla ya kuuzwa sokoni?
Neema anaweza kukuambia kama, katika uzoefu wake, hayo ni makadirio mazuri. Ni simulizi yake, uzoefu wake ambao unatafuta.
3. Andika maswali yako—epuka maswali ya kuongoza.
Maswali yasiyo ya kuongoza ni maswali ya wazi ambayo huondoa upendeleo au matarajio ya anayehoji. Yameundwa ili kuruhusu wahojiwa kupata uhuru wa kujibu kwa njia yoyote wanayochagua. Maswali yenye ufanisi zaidi yasiyo ya uongozi yanaongoza kwenye majadiliano ambayo mara nyingi yanafichua maarifa na mawazo ambayo anayehoji anaweza kuwa hajawahi kuyafikiria. Katika maswali yasiyo ya uongozi, mhojiwa halazimishwi kukubaliana au kutokubaliana na anayehoji, wala mhojiwa hashawishiwi na mapendekezo ya anayehoji.
Huu hapa ni mfano wa mstari wa maswali unaojumuisha maswali ya wazi ambayo mtu wetu aliyekuwa anahoji alipaswa kutumia wakati anamhoji Neema.
Je, unaweza kueleza jinsi shamba lako linavyoonekana?
Mavuno yako ya mahindi yalikuwaje mwaka huu?
Ni mambo gani yaliyoathiri mavuno?
Unatumia mbegu za aina gani Neema?
Walifanyaje?
Nieleze jinsi wewe na Godfrey mnavyopanda na kuvuna mahindi.
Je wewe na Godfrey mnafanyaje maamuzi yenu ya kilimo?
Je, ni muhimu kwako kufanya kazi kama timu?
Je, unajua kama ulipata hasara ya mazao wakati wa mavuno?
Unadhani sababu zake ni zipi?
Unahisi nini kuhusu mbinu mbalimbali za uvunaji ambazo baadhi ya wakulima wanajaribu?
Kwa nini umechagua kuhifadhi mahindi yako kwenye mifuko?
Ulijifunzaje kufanya hivyo?
Ni njia gani zingine za kuhifadhi umezisikia?
Je, kuna faida au hasara gani kwa kila mfumo unavyouelewa?
Je, una mipango gani ya baadaye ya kuvuna na kuhifadhi?
Haya yote ni maswali ya wazi na ni mwanzo mzuri wa swali lako. Lakini kuna mambo mengine ya kuzingatia wakati wa kuunda maswali bora.
4. Andaa maswali ambayo ni mahususi, kulingana na utafiti wako.
Usiulize maswali ya jumla. Fanya swali liwe mahsusu. Kwa mfano, usiulize swali kama vile,
"Ni ipi njia bora ya kukabiliana na matatizo ya wadudu katika mahindi?"
Kuna aina nyingi za wadudu wanaoharibu mimea ya mahindi na mahindi yaliyohifadhiwa. Kwa hiyo, kwa kweli, jibu la kweli zaidi kwa swali hilo lingekuwa, “Inategemea.” Kwa hivyo hakikisha swali lako ni mahsusi, kwa mfano:
"Ni ipi njia bora ya kukabiliana na viwavi jeshi katika mahindi wiki sita baada ya kupanda?"
"Unafanya nini kuzuia wadudu kwenye mahindi yako yaliyovunwa?"
Kamwe usitumie maneno "inapendekezwa" au "sahihi" katika swali. Kwa mfano,
"Je, unatumia ghala la chuma linalopendekezwa kuhifadhi mahindi yako?"
Tatizo la kutaja swali lako kwa njia hii ni kwamba baadhi ya watu ambao hawatumii chaguo la kuhifadhi linalopendekezwa wanaweza kukuambia kwamba wanafanya hivyo, au wanapanga kufanya hivyo, kwa sababu hawataki kujionyesha wapo katika upande ambao haukubaliani au hautumii njia hiyo. Vilevile, Neema anaweza kuamini kuwa anafanya kile ambacho kimependekezwa lakini hakuelewa kikamilifu mchakato uliopendekezwa. Anayehoji lazima awe mwangalifu asichukue maarifa kwa kudhania. Maswali ya wazi hupunguza hatari ya kudhania.
Kwa sababu ya utafiti wako, utakuwa na ufahamu wa njia mbalimbali za kukabiliana na tatizo fulani, kwa mfano, tatizo la wadudu au tatizo la rutuba ya udongo au kuvuna. Ukitumia mifano maalum itakupa majibu mahususi.
Je, unafikiri nini kuhusu wazo kwamba wakulima katika eneo lako wanakusanyika ili kununua mashine moja ya kuvuna mashine ambayo kila mtu anaweza kutumia kwa zamu?
Kuwa mahususi kuhusu kile unachotaka kujua huwasaidia wanaohojiwa kama vile Neema kujibu swali vizuri zaidi kwa sababu anajua hasa unachotaka. Pia itawapa wasikilizaji wako taarifa bora na mahususi zaidi.
5. Tayarisha aina tofauti za maswali
Kila mahojiano yanahitaji mchanganyiko unaofaa wa 1) maswali ambayo yanasaidia kupata taarifa, na 2) maswali ambayo yanaangazia tabia au utu na hisia za mhojiwa. (Tafadhali kumbuka kuwa, ingawa ni muhimu kuuliza aina zote mbili za maswali, kwa uhalisia, maswali binafsi mara nyingi yataonyesha taarifa na tabia/utu/hisia.)
Kufikia sasa, maswali yetu mengi ya mfano yamekuwa yakitafuta ukweli. Tulimuuliza Neema kuhusu mazao yake, mbinu za kuvuna, na njia za kuhifadhi. Lakini hatujui mengi kuhusu yeye ni nani kama mtu, kama mke, mama, na mjasiriamali. Hatujui kuhusu matumaini na ndoto na hofu zake.
Sasa, ili kuwa na uhakika, huenda tusihitaji mengi ya hayo kwa programu yetu. Lakini watangazaji wa muda mrefu watakuambia kwamba wasikilizaji wako watasikiliza kwa makini zaidi watu ambao wanaweza kuwa na hisia zinazoendana au kufanana. Wanakuwa majirani na marafiki na mara nyingi wanakuwa vielelezo, wakishirikishana masuala ya kilimo. Watu hawa wa kuigwa wanatakiwa kuakisi jamii wanayotoka.
Maswali unayouliza, kama yalivyoonyeshwa katika sampuli ya maswali hapo juu, yanamsaidia mhojiwa kusimulia hadithi yake. Pamoja na maswali yanayosaidia hadhira kutambua na kuwa na huruma kwa mhojiwa (anapoishi, ni nani katika familia yake, shamba lake ni kubwa kiasi gani, analima mazao gani, matumaini na ndoto zake), unahitaji kumfanya aelezee vikwazo au matatizo anayopaswa kuyatatua. Watafahamika na wengi katika hadhira yako.
Ifuatayo ni njia ya kufikiria juu ya muundo wa mahojiano mengine na aina ya maswali ya kuuliza. Mara nyingi hufafanuliwa kama safu ya simulizi, yenye kusimulia hadi kilele. Kilele huja pale mhojiwa anapoeleza jinsi tatizo lilivyotatuliwa. Hakikisha kuwa maswali yako yamekamilika, himiza maelezo ya kina, na umsaidie mhojiwa kusimulia hadithi yake kwa mpangilio unaoeleweka.
Hapa kuna masuala ya kuzingatia katika maswali yako.
• Ni hatua gani walijaribu kujaribu kutatua tatizo,
• Jinsi na kwa nini baadhi ya mambo hayakufanya kazi,
• Ni hatari gani zilihusika,
• Ni chaguzi gani walizokuwa nazo,
• Ni chaguzi gani walizofanya na kwa nini walizifanya,
• Ni wakati gani waliona kuwa wamepata suluhu ya tatizo lao,
• Nani aliwasaidia, na
• Jinsi hali yao ilivyobadilika, pamoja na hali ya familia na jamii yao.
Hadithi inapoendelea, ni muhimu kwa hadhira kujifunza jinsi mhojiwa anavyohisi kuhusu kile kinachotokea. Uliza maswali yanayodhihirisha hilo. Kwa kawaida, maswali kama haya huanza na "Unahisije kuhusu ..." Lakini kuna njia zingine. Kuwa mwangalifu, hata hivyo, usiulize maswali ya hisia kama vile:
Lazima ulikuwa na hasira wakati ...
Au
Ulikuwa na furaha gani wakati ...?
Pia, baadhi ya wahojiwa wanaweza kusitasita kuzungumza juu yao wenyewe na hisia zao. Utahitaji kujenga uaminifu nao kabla ya kupata maswali ambayo yanatafuta hisia.
Hapa kuna baadhi ya maswali kwa Neema ambayo yanatafuta kuonyesha tabia na hisia zake.
Ulijisikiaje mwanzoni mwa msimu wa kupanda?
Ilikuwaje kwako na Godfrey ulipogundua ni kiasi gani cha mahindi kilipotezwa na viwavi jeshi?
Je, unaweza kueleza siku ya kwanza ambayo mwanao aliweza kukusaidia kwenye mavuno?
Je, una ndoto gani kwa mustakabali wa shamba lako?
Wasikilizaji wengi watakubaliana na maswali haya—na pengine majibu ambayo Neema atatoa. Watamfahamu na watataka kusikia anachosema kuhusu uzoefu wake katika kilimo.
6. Kuwa tayari kuuliza maswali mazuri ya kufuatilia
Sawa na swali lililo wazi, mara nyingi zaidi mhojiwa wako hatakupa kila kitu unachohitaji katika kila jibu.
Kama tulivyoona, kadiri swali lilivyo maalum, ndivyo jibu mahususi zaidi nalo huwa. Lakini mara nyingi kuna maelezo yaliyoachwa, kudadisi hisia, maelezo ya kutolewa.
Unapaswa kuwa tayari kuuliza maswali ya kufuatilia. Hiyo ina maana kwamba unapaswa kusikiliza kwa makini sana anachosema mhojiwa.
Hapa ndipo kuwa na mstari wa maswali uliotayarishwa mapema kunasaidia sana.
Ikiwa una swali kuu linalofuata tayari akilini, sio lazima ufikirie juu yake. Unaweza kuzingatia kabisa jibu la swali lililotangulia-ilikuwa na maana? Je, lilienda mbali vya kutosha? Je, lilikuwa na maelezo yote? Je, kuna maudhui ya kihisia ya kutafuta? Hapa kuna mfano:
Swali kuu:
Je, zao la mahindi la mwaka huu lilikuwaje, Neema?
Maswali yanayoweza kufuata kulingana na jibu lake:
Unaweza kulinganisha na mwaka jana?
Kwa nini mwaka jana ulikuwa bora zaidi?
Je, unaweza kueleza hilo?
Ulijisikiaje baada ya mavuno ya mwaka huu?
Kuuliza maswali ya ufuatiliaji hakuhitaji kusikiliza tu, bali kubadilika. Unaweza kuwa na orodha yako ya maswali kwenye daftari au simu yako, lakini ikiwa mazungumzo yataelekea kwenye mwelekeo usiopangwa, unahitaji kuwa na kitu cha kuuliza. Ingawa kupanga ni muhimu, ndivyo kuitikia kwa kile unachosikia.
Wakati mwingine maswali ya ufuatiliaji lazima yatoe changamoto kwa jibu la mhojiwa. Wakati mwingine, ufuatiliaji unaweza kukusaidia kuelewa vyema jibu tata. Ikiwa hujui kile ambacho mtu anamaanisha, ni bora kusema, "Tafadhali nielezee." Au “Unaweza kunipa mfano?” Mara nyingi unapata mafasi moja tu kwenye mahojiano.
Hapa kuna mbinu tatu za kuuliza maswali ya ufuatiliaji
A. Uliza swali lako tena, tofauti kidogo. Usiogope kuuliza swali moja mara mbili. Iwapo unamhoji mtu na mtu huyo anageukia swali la kwanza au hatoi jibu halisi, unaweza kusema, “Hebu nikuulize swali hili kwa njia nyingine…” Hii ni nzuri kwa sababu unamjulisha mhojiwa kuwa humruhusu kwenda nnje ya swali ulilouliza, lakini unawaruhusu kuoana angalau kuwa labda swali lako la kwanza halikuwa wazi vya kutosha.
Tahadhari: Hakikisha umebadilisha jinsi unavyotamka swali hili la pili, vinginevyo linaweza kuonekana kuwa gumu. Jambo kuu ni kuuliza swali kwa njia nyingine, na kusema kwamba unafanya hivyo.
B. Unganisha majibu ya mhojiwa wako kwa kusikiliza kwa makini.
Mkakati mmoja mzuri wa kuelewa anachosema mhojiwa ni kuunganisha majibu yao na jambo alilosema awali. Hii sio juu ya kujaribu kumnasa mtu kwa uwongo, lakini badala yake juu ya kuunganisha nukta kati ya majibu yao. Unaweza kusema kitu kama, "Loo, ni kama wakati ...?" au, “Je, ndivyo ulivyomaanisha hapo awali uliposema…?” Pamoja na kukusaidia kumwelewa mtu huyo vizuri zaidi, inamwambia kwamba unamsikiliza kikweli, na kwa hakika inatoa ufahamu wa maana kwa mtu huyo kwa kuonyesha uhusiano ambao huenda hajauona. Inakuruhusu kuunganisha habari badala ya kuisikia tu.
Tahadhari: Kutumia njia hii kupita kiasi kunaweza kukufanya uonekane kama mpelelezi wa polisi anayejaribu kukamata mhalifu kwa uwongo na kulazimisha kuungama. Epuka kusema mambo kama vile, "Lakini sivyo ulivyosema awali ..." Hii inahusu zaidi kusanisi kuliko kuhoji.
C. Uliza swali kuhusu maana ya jibu lao.
Watu wanapojibu swali bila kufichua hasa, au kwa kutoa jibu “salama” sana, unafanya nini? Badala ya kukubali majibu yasiyo ya kufichua usoni, tafuta kumwelewa mtu huyo kwa kuuliza kuhusu maana ya majibu yake. Kwa mfano:
Neema, umesema shamba lako lipo katika mpangilio na nadhifu. Ina maana gani kwako kuwa na shamba kama hili?
Tunajua Neema lazima afanye bidii sana kuelezea juu ya jinsi shamba linavyoonekana. Inaweza kukufanya ujiulize anajitolea nini kwa ajili ya kufanya shamba kuonekana hivyo.
Swali linalofuata la ufuatiliaji linaweza kuwa:
Je, unapataje wakati wa kufanya yote hayo?
Tahadhari: Unapouliza kuhusu wanachomaanisha, epuka kuuliza maswali ya kuongoza. Badala yake, kuwa na shauku ya kweli kuhusu kile wanachosema na kupata maana ya majibu yao.
Kuna sababu nyingine za kuuliza maswali ya kufuatilia, na huathiri aina ya maswali utakayouliza. Kwa mfano, unaweza:
• Muulize mhojiwa afafanue maana ya majibu yake.
• Uliza mifano inayoonyesha jambo wanalojaribu kueleza.
• Uliza, “Hii ina maana gani kwa ___?”
• Toa maoni yanayopingana (kwa mfano, “Baadhi ya watu wanasema kuwa na shamba nadhifu na lenye mpangilio mzuri ni kupoteza muda …”) na waulize wanafikiri nini kuhusu wazo hilo.
Ni maswali ya ufuatiliaji ambayo hufanya mahojiano mazuri kuwa mahojiano bora. Maswali mazuri ya ufuatiliaji hutoa maelezo mazuri, tabia, na hisia.
Pointi zingine
Mapendekezo hapo juu ya kuuliza maswali bora yanaweza kutumika kwa mahojiano yoyote. Wakati wa kumhoji mwanasiasa, kwa mfano, maswali ya wazi ambayo ni mahususi sana hufanya iwe vigumu kwa mwanasiasa kujitenga na jibu moja kwa moja. Na ikiwa watachagua kutojibu moja kwa moja, mhojiwa ana chaguzi mbalimbali. Wangeweza kusema “Hebu niweke swali kwa njia nyingine…” au kuuliza “Kwa nini hujibu swali?” Ni kweli, lakini inaweza kuwa swali muhimu.
Huenda usiweze kuuliza maswali kuhusu tabia na hisia kwa mwanasiasa au mtaalamu kwa sababu unatafuta majibu mahususi. Hata hivyo, wanasiasa na wataalam ni watu pia na kujifunza zaidi kuwahusu kwani watu wanaweza kuwasaidia wasikilizaji kuelewa vyema wanachosema.
Ni wapi pengine ambapo ninaweza kujifunza kuhusu kuuliza maswali bora zaidi?
BBC Academy, undated. Ask clear, simple interview questions: Jeremy Paxman. https://rl.talis.com/3/lsbu/items/00BFC3CA-38DA-9642-EE3C-07D097D5D010.html
Columbia University, undated. Interviewing principles. http://www.columbia.edu/itc/journalism/isaacs/edit/MencherIntv1.html
Davis, Richard, 2014. Tactics for Asking Good Follow-up Questions. https://hbr.org/2014/11/tactics-for-asking-good-follow-up-questions
Farm Radio International, 2016. How to conduct an effective interview. https://training.farmradio.fm/how-to-conduct-an-effective-interview/
Farm Radio International, 2017. Interviewing experts: Best practices for broadcasters and experts. https://training.farmradio.fm/how-to-interview-experts-best-practices-for-broadcasters-and-experts/
Halbrooks, Glenn, 2019. Conducting a good television interview. https://www.thebalancecareers.com/tv-interview-tips-for-news-media-professionals-2315424
MediaCollege.com, undated. Leading Questions. https://www.mediacollege.com/journalism/interviews/leading-questions.html
Pizarro, A. G., 2015. Qualitative Interviewing: 3 Mistakes to Avoid in Question Formulation. http://simplyeducate.me/2015/02/08/qualitative-interviewing-3-mistakes-to-avoid-in-question-formulation/
Shukrani
Imechangiwa na: Dick Miller, mtayarishaji wa kujitegemea wa redio, mkufunzi, na mtayarishaji wa makala wa zamani wa CBC Redio, mhadhiri katika Warsha, Shule ya Uandishi wa Chuo Kikuu cha King's College.
This resource was supported with the aid of a grant from The Deutsche Gesellschaft für Internationale Zusammenarbeit GmbH (GIZ) implementing the Green Innovation Centre project. It was translated thanks to generous donations to Farm Radio International.