Jinsi kituo chako kinaweza kusaidia kuzuia kuenea kwa UVIKO-19 na kuwaweka wasikilizaji wako salama

Usuli

UVIKO-19 ni ugonjwa wa virusi wa kuambukiza ambao umekuwa janga (umeenea kote nchini kwako) na sasa ni janga kubwa (limeenea katika nchi nyingi).

Kituo chako cha redio kinaweza kuchukua jukumu muhimu. Unaweza kusaidia kuwafanya wasikilizaji wako kuwa salama, na unaweza kuwasaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu!

Wakati ambapo mikutano katika vikundi si salama, kituo chako kinaweza kuwa jukwaa muhimu la majadiliano na msaada kuhusu UVIKO-19 katika eneo lako.

Fikiria hukusu hili.

  • Unatangaza kwa kutumia lugha ya nyumbani.
  • Umepata heshima kwa wasikilizaji wako kwa miaka mingi kwa programu yako ya kuaminika na ya ukweli.
  • Wewe huwapa wasikilizaji nafasi ya kuelezea wasiwasi wao mara kwa mara hewani.

Hakuna shirika ambalo lina nafasi nzuri ya kutoa huduma hii muhimu kwa wakati huu!

Mwongozo huu utakusaidia kuzalisha na kutangaza vipindi bora vya redio ili kudhibiti vizuri UVIKO-19 katika eneo lako. Pia utakuunganisha na mashirika ambayo yanaweza kukusaidia. Mwongozo unajumuisha:

  1. UVIKO-19 ni nini? Inaathiri watu gani? Inaeneaje? Ni nani anayeathirika zaidi (au aliye katika mazingira hatarishi ya kuathirika) wakati wa janga hilo?
  2. Ipi ni miongozo ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na miongozo ya kitaifa ya afya ya kudhibiti UVIKO-19?
  3. Kutoa kipaumbele kwa sauti za wanawake na maoni yao.
  4. Ni nini madhumuni sita ya programu bora ya UVIKO-19?
  5. Changamoto gani kituo chako cha redio kinaweza kukutana nazo?
  6. Unaanzaje?

Utapata viambatisho vifuatavyo:

  • Kiambatisho 1: Ni wapi tunaweza kupata msaada zaidi kutoka Farm Radio International na vyanzo vingine kutengeneza programu nzuri ya UVIKO-19?
  • Kiambatisho 2: Sampuli ya vipengee vya programu na vitu vinavyoonyesha madhumuni sita ya programu bora ya UVIKO-19.
  • Kiambatisho 3: Mfano wa shiti ya kuongoza kipindi kinachohusu mpango wa UVIKO-19.

Maelezo

1. UVIKO-19 ni nini?

UVIKO-19 ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi. Dalili za kawaida ni pamoja na homa, changamoto ya kupumua, uchovu, na kikohozi kikavu. Watu wengi walioambukizwa hawana dalili na hawajisiki kuwa wagonjwa. Watu wengi hupona bila matibabu maalum. Walakini, wengi huwa wagonjwa mahututi, na asilimia ndogo ya watu walioambukizwa hufariki.

UVIKO-19 huathiri kina nani?

Mtu yeyote anaweza kupata UVIKO-19. Watu wazee na watu walio na shida za kiafya kama shida za moyo, ugonjwa wa kisukari, au shinikizo la damu wana uwezekano wa kuugua sana. Walakini, UVIKO-19 pia huambukiza vijana. Kila mtu aliye na homa, kikohozi, au changamoto ya kupumua anapaswa kukaa mbali na watu wengine, kufuatilia dalili zao kwa uangalifu, kupumzika, na kula chakula bora chenye afya.

Watoto na vijana wanaweza kuambukizwa kama kundi lingine lolote la umri, lakini wana uwezekano mdogo wa kuugua sana. Wanaweza pia kueneza ugonjwa.

UVIKO-19 inaeneaje?

Ugonjwa huu unaambukiza sana! Unaenea kwa njia tatu:

  • wakati mtu aliyeambukizwa anakohoa, anapiga chafya, anaongea, anapiga kelele, au anaimba, na mate yake yenye virusi yanakutana na mdomo, pua au macho ya mtu aliye karibu. Kumbuka kuwa tafiti za kisayansi zimeonyesha kuwa mate kawaida husafiri mita 1 au chini ya hapo, lakini yanaweza kusafiri hadi mita 2. Hii ndio njia kuu ya kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya UVIKO-19.
  • wakati vijidudu vidogo vya virusi vinapopeperushwa hewani na kukutana na mdomo, pua, au macho ya mtu.
  • mate ya mtu aliyeambukizwa yanapotua juu ya nyuso (kwa mfano chakula, zana, fanicha, mavazi) ambayo baadaye huguswa na mtu mwingine ambaye baadae hugusa mdomo wake, pua, au macho.

Kwa habari zaidi, angalia ugonjwa wa virusi vya Korona (UVIKO-19): Inaambukizwaje?

Watu wengi ambao wana ugonjwa hawaonyeshi dalili na wanaendelea na maisha yao ya kila siku na mwingiliano na watu wengine. Unaweza kuwa na virusi na usiwe mgonjwa! Lakini bado unaweza kusambaza virusi kwa wengine. Ndio maana ni muhimu sana kwa kila mtu kufuata mwongozo wa kitaifa wa afya kuzuia UVIKO-19.

Hadi leo hakuna tiba ya matibabu ya UVIKO-19, ingawa kuna dawa zingine ambazo hupunguza dalili na hupunguza uwezekano wa kufariki. Ikiwa dalili zinazidi kuwa mbaya, mtu anapaswa kuwasiliana na kituo cha matibabu ambacho kinashughulikia watu walio na UVIKO-19.

Kuanzia Februari 2021, chanjo kadhaa zimeidhinishwa katika nchi mbalimbali, na nyingine zaidi zinatengenezwa. Hizi zinaweza kupatikana kwa wingi ndani ya miezi ijayo au miaka michache, ingawa usambazaji kwa maeneo ya vijijini unaweza kuwa polepole. Lakini, bila kujali maendeleo ya chanjo ya idadi ya watu, itaendelea kuwa muhimu kuchukua tahadhari kama vile kukaa umbali kati ya mtu na mtu na kuvaa barakoa kwa miezi kadhaa au hata zaidi.

 

2. Miongozo ya Kiafya ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na miongozo ya kitaifa ya Afya ni nini?

Miongozo ya kiafya ni shughuli ambazo kila mtu anapaswa au lazima kufanya ili kubaki salama na kuzuia kuenea kwa UVIKO-19. Kwa kuwa athari ya virusi kwa jamii hubadilika kwa muda, miongozo ya afya pia inaweza kubadilika kwa muda.

Baadhi ya miongozo imeundwa na mashirika ya afya ya kimataifa, na mingine na mashirika ya kitaifa. Baadhi ya miongozo ina nguvu za kisheria na miongozo mingine ni mapendekezo tu.

Miongozo ifuatayo imechukuliwa kutoka katika miongozo ya Shirika la Afya Ulimwenguni. Kuna makubaliano yaliyoenea juu ya njia zifuatazo za kinga.

Nyumbani

  • Kaa nyumbani kadri iwezekanavyo.
  • Kohoa au piga chafya kwenye kiwiko au kitambaa.
  • Osha mikono yako kwa maji na sabuni mara kwa mara (mara nyingi kwa siku). Kumbuka kuwa ikiwa sabuni ya kununua haipatikani, sabuni iliyotengenezwa nyumbani inakubalika. Ikiwa hakuna sabuni inayopatikana, sugua mikono kwa nguvu kwa kutumia maji tiririka. Lakini fanya hivyo tu kama njia ya mwisho kabisa - kutumia sabuni daima ni bora zaidi.
  • Osha mara kwa mara nyuso zozote ambazo watu katika nyumba yako hugusa.
  • Epuka kugusa mdomo, pua, na macho.
    Usialike watu wengine isipokuwa familia yako ya karibu nyumbani kwako.
  • Ikiwa mtu atakuja nyumbani kwako, vaa barakoa na kaa umbali wa mita 1-2 kutoka mahali walipokaa.
  • Ikiwa mwanafamilia ana homa, kikohozi, au anapumua kwa shida, muweke nyumbani na utafute matibabu pale yanapopatikana. Ikiwa mtu katika familia yako ameambukizwa au ana dalili za maambukizi ya UVIKO-19, inashauriwa kila mtu katika familia hiyo abaki nyumbani.
  • Ikiwa unamtunza mtu mgonjwa, vaa glavu, barakoa, na kunawa mikono mara nyingi. Epuka kugusa uso wako.

Uangalizi wa watoto

  • Wahimize watoto kunawa mikono yao mara kwa mara. Agiza watoto wasiguse nyuso zao. Hakikisha kwamba watoto huosha mikono kabla ya kula.
  • Ni sawa kwa watoto kucheza kwa uhuru na watoto wengine na watu wazima katika nyumba zao.
  • Ikiwa watoto wamekutana na mtu aliye na virusi vya korona au ikiwa wanaonyesha dalili, wanapaswa kufuata mwongozo huo huo juu ya kukaa karantini na kujitenga kama watu wazima. Ni muhimu sana kwamba watoto waepuke kukutana na watu wakubwa na wengine walio katika hatari ya kupata magonjwa.

Nnje kwenye jamii

  • Vaa barakoa inayofaa au kitu kingine cha kufunika uso kinachofunika mdomo wako na pua.
  • Kaa umbali wa mita 1 hadi 2 kutoka kwa watu wengine.
  • Nawa mikono mara tu baada ya kununua bidhaa sokoni, na unaporudi nyumbani.
  • Epuka salamu zilizozoeleka zinazojumuisha kugusana mwili kama vile kukumbatiana, kupeana mikono, na busu. (Badala yake, punga mkono, inamisha kichwa, pinda, au tumia maneno tu.)
  • Epuka mikutano yote ya ndani.
  • Kwenye mikutano ya nje (mikutano ya kidini au huduma, mikutano ya vikundi vya wanawake, mikutano ya shirika la wakulima, n.k.), hakikisha kila mtu ana barakoa au kifunika uso kingine cha uso, na hakikisha watu wamekaa kwa umbali wa mita 1 hadi 2.
  • Ikiwezekana, wahimize watoto wako kukaa mita 2 mbali na marafiki wakati wa kucheza na wacheze nnje.
  • Wahimize watoto kunawa mikono mara kwa mara. Agiza watoto wasiguse nyuso zao. Hakikisha kwamba watoto huosha mikono kabla ya kula.

Hii ni miongozo ya jumla. Katika nchi yako, serikali itatoa seti ya miongozo ya kitaifa ya afya kwa raia na mashirika kufuata. Ngazi nyingine za serikali (kwa mfano, mikoa, majimbo, na wilaya) zinaweza pia kutoa mwongozo. Ni muhimu kituo chako cha redio kukuza/kusambaza miongozo inayotolewa na serikali yako. Tafadhali kumbuka kuwa miongozo inapaswa kuzingatiwa kuwa ya kiwango cha chini: watu binafsi, mashirika, wafanyabiashara wanaweza kutaka kufuata miongozo mingine zaidi ya kinga.

* Tafadhali kumbuka pia kuwa, kwasababu asilimia kubwa ya watu ambao wameambukizwa na UVIKO-19 hawaonyeshi dalili, ni muhimu kufuata miongozo hii ikiwa watu wanaonyesha dalili za kuambukizwa au la.

3. Kutoa kipaumbele kwa sauti za wanawake na maoni yao

Programu zote za UVIKO-19 zinapaswa kujumuisha sauti na mawazo ya wanawake. Kiutamaduni wanawake hufanya majukumu mengi katika familia na jamii: wanaweka viwango vya afya nyumbani, ndio wanunuzi wakuu na wauzaji katika masoko ya chakula, wanawatunza wagonjwa nyumbani, na ndio wafanyakazi wakuu walio mstari wa mbele katika vituo vya afya ambavyo vinatibu wagonjwa wa UVIKO-19. Jitihada zao zinapaswa kutambuliwa na kuungwa mkono, na wanaume na wavulana wanapaswa kuhamasishwa kuchangia zaidi katika majukumu ya familia na jamii. Kituo chako pia kinapaswa kuhimiza mamlaka za ndani kushirikisha wanawake katika kila hatua ya kufanya uamuzi wa jinsi ya kushughulikia changamoto zinazohusiana na UVIKO katika eneo lako la utangazaji.

Shirikisha ujumbe ambao unasisitiza tabia nzuri inayowaweka watoto na wanawake salama majumbani mwao. Kwa mfano, wanawake na watoto wanaweza kupata unyanyasaji nyumbani wakati wa shida ya kiafya kama UVIKO-19. Kama hatua za afya ya umma zinazohusiana na UVIKO-19 zinasababisha jamii "kujifungia" kuongezeka kwa dhiki za kiuchumi na kisaikolojia, vurugu nyumbani zinaweza kuongezeka. Njia za kusaidia na kuripoti kama vile shule, washauri, na vikundi vya jamii vinahitajika zaidi kuliko wakati wowote, lakini zinaweza kuvurugwa na janga hilo. Kituo chako kinaweza kushirikisha habari juu ya msaada kama vile nambari za msaada kwa wanawake / nambari za simu, pamoja na huduma zinazotoa msaada kwa wazazi / walezi, pamoja na mwongozo wa jinsi ya kuripoti unyanyasaji unaoshukiwa, pamoja na unyanyasaji wa kijinsia.

4. Madhumuni sita ya programu bora ya UVIKO-19

Kuna madhumuni sita ya programu bora ya UVIKO-19. Yanapaswa kujumuishwa katika kila sehemu ya programu yako ya kila siku au ya kila wiki ya UVIKO-19.

Dhumuni la 1) Toa habari sahihi juu ya hali ya UVIKO-19 katika eneo lako na nchi yako. Hii ni pamoja na kukuza mipango ya serikali inayounga mkono watu binafsi au biashara wakati wa UVIKO. Programu kama hizo hutoa msaada wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja. Kwa mifano, angalia Kiambatisho 2.

Dhumuni la 2) Sahihisha habari za kughushi, uwongo, na habari zingine potofu. (Tazama Changamoto # 3 hapa chini)

Dhumuni la 3) Tangaza na ufafanue miongozo ya afya mara kwa mara, kwa lugha ya wasikilizaji wako. Tangaza njia mbadala za ulinzi wakati, kwa mfano, ni vigumu kupata sabuni ya kunawa mikono, au wakati ambapo kukaa umbali kati ya mtu na mtu ni vigumu.

Dhumuni la 4) Wape viongozi wa eneo husika nafasi ya kuonyesha uongozi katika juhudi za kusaidia kuzuia kuenea kwa UVIKO-19.

Dhumuni la 5) Wape wasikilizaji nafasi ya kusema kuhusu maoni yao kuhusiana na kufuata miongozo-na kuhakikisha maoni yao yanashughulikiwa na maafisa wenye ujuzi, wataalam wa afya, na wasikilizaji wengine.

Dhumuni la 6) Saidia wasikilizaji na mashirika wanapofanya kazi kushinda changamoto na kupitisha miongozo ya afya.

 

5. Changamoto gani kituo chako cha redio kinaweza kukutana nazo?

Uzalishaji na utangazaji wa programu ya UVIKO-19 haitakuwa rahisi au wa moja kwa moja. Lakini ni huduma muhimu, na mwishowe, itaongeza heshima ambayo wasikilizaji wako-na jamii yako-wanayo kwa kituo chako. Hapa kuna changamoto ambazo unahitaji kuwa tayari kukutana nazo.

Changamoto ya 1) Rasilimali: Huenda ukahitaji kupeana rasilimali zingine za kituo na muda wa hewani ambao hutumiwa sasa kwa programu zingine. Kwa hivyo, ni muhimu kwa kila mtu kukubali kuwa programu ya UVIKO-19 ni huduma ambayo ni ya kipaumbele kwa kituo kutoa. Kituo chako pia kinaweza kupoteza wafanyakazi kwasababu ya kufungiwa ndani/vizuizi vya kutembea, na unaweza kushindwa kusambaza pia habari kwa sababu ya kukatika kwa umeme na kupoteza uwezo wa kusambaza programu yako kwa muda mfupi.

Changamoto ya 2) Kukuza na kutafsiri miongozo ya serikali: Ikiwa serikali yako ina mpango kamili wa kitaifa wa kupambana na UVIKO-19, jukumu la kituo chako cha redio ni kusaidia kutekeleza mpango huo. Hii inajumuisha:

  • kutoa habari sahihi juu ya miongozo ya kitaifa ya afya, na
  • kusaidia wasikilizaji wako wanapotekeleza miongozo hiyo ya kitaifa ya afya.

Hii haimaanishi kuwa huwezi kutafsiri jinsi miongozo inaweza kutekelezwa vyema katika eneo lako la kusikiliza. Mifano miwili:

  • Mwongozo wa kitaifa unaweza kuhitaji kila mtu kusugua mikono yake mara nyingi kwa siku kwa sabuni na maji. Walakini, sabuni inaweza kuwa na uhaba sana katika sehemu ya eneo lako la kusikiliza. Tafuta watu ambao wanaweza kuzungumza juu ya wapi pa kupata sabuni. Unaweza pia kupata watu (pamoja na maafisa wa afya) ambao wanaweza kuzungumza juu ya jinsi ya kutengeneza sabuni, jinsi ya kutengeneza kituo cha umma cha kuoshea mikono, na pia juu ya njia mbadala bora za kusugua mikono na sabuni. Ikiwa upatikanaji wa maji ni changamoto, wahoji watu (pamoja na maafisa wa afya) ambao wanaweza kuzungumza juu ya suala hili na pia jinsi ya kufuata mwongozo wa usafi bila kupata maji safi. (Bonyeza hapa kujua kuhusu utengenezaji wa sabuni.)
  • Mwongozo wa kitaifa unaweza kusema kwamba kila mtu anapaswa kuvaa barakoa akiwa karibu na watu wengine. Walakini, kunaweza kusiwe na barakoa zozote zinapatikana kwenye maduka katika sehemu za eneo lako la matangazo. Pata watu ambao wanajua wapi pa kupata barakoa, na pia jinsi ya kutengeneza barakoa nzuri.

Changamoto ya 3) Kukabiliana na uwongo na habari potofu: Kuna tovuti na mashirika na watu binafsi ambao wanasema kuwa UVIKO-19 ni uwongo. Pia kuna hadithi nyingi juu ya jinsi virusi vinavyoenea. Wanasayansi wanathibitisha kwamba UVIKO-19 ni ugonjwa wa kuambukiza sana ambao unaweza kuharibu maisha na uchumi. Wafanyakazi wa kituo, hata hivyo, wanaweza kulazimika kukabiliana na upinzani na uhasama kutoka kwa raia ambao wanaamini UVIKO-19 ni uwongo. Hakikisha kituo chako kinasaidia na kutetea wafanyakazi wako kadri kinavyokuza miongozo ya afya.

Changamoto ya 4) Kukabiliana na vikwazo vinavyosababishwa na ugonjwa: Wakati programu ya UVIKO-19 ingefaidika sana kutokana na majadiliano ya jopo la ana kwa ana na mahojiano ya studio, na pia kwa kutembelea vijiji vya mbali, shughuli hizi zinaweza kuwa haziwezekani kwasababu ya tishio kwa wafanyakazi wako na kwa watu unaowahoji. Walakini, waandaaji wabunifu wa programu wataweza kufanya kazi wakati wa vizuizi hivi. (Bonyeza hapa kwa mwongozo wa FRI juu ya kufanya majadiliano ya paneli kupitia njia ya simu.)

Changamoto 5) Kuweka wafanyakazi wako na wageni salama: Kituo cha redio kawaida huleta wafanyakazi na raia pamoja kufanya kazi katika sehemu iliyofungwa. Kwa bahati mbaya, hii ni njia nzuri ya kueneza UVIKO-19! Fuata miongozo hii kufanya kituo kuwa sehemu salama:

  • Fanya utangazaji, mahojiano na uhariri eneo la nje kadri iwezekanavyo, ukishirikisha mtu mmoja tu kwenye mashine moja ya kurekodi. Weka kipaza sauti cha mhojiwa kwenye kebo ambayo itawaweka umbali wa mita 1 hadi 2 kutoka kwa muhojiwa.
  • Hakikisha wafanyakazi wote na wageni wote wanavaa barakoa wakati wote na wanafanya kazi angalau mita 1 hadi 2 kutoka kwa kila mmoja.
  • Fanya mpango mkakati wa kusafisha kituo chako mara kwa mara. Futa vipasa sauti vyote, n.k na dawa ya kuua vimelea wakati wa matumizi. (Usiweke dawa ya kuua vimelea moja kwa moja kwenye kipaza sauti, kinasa sauti, au bodi ya kudhibiti. Nyunyizia kwenye kitambaa na kisha ufute vifaa na ragi hiyo.)
  • Hakikisha kwamba mfanyakazi au mgeni yeyote anayeonyesha dalili za UVIKO-19 anaepuka kuja kituoni- au hata kufanya kazi nnje.
  • Badilisha mahojiano ya studio na kufanya mahojiano ya simu.
  • Kuwa msaada kwa wafanyakazi ambao hawawezi kufanya kazi kwa sababu lazima waangalie wanafamilia ambao wana UVIKO-19, na pia wafanyikazi walioathiriwa na vizuizi vya kutembea, kufungwa kwa shule, magonjwa, n.k.

6. Uaanzaje?

Kuanza 1) Thibitisha idhini ya wasimamizi wa kituo kuhusu dhana ya programu, kwa muda wa programu, na kwa matangazo ya kila siku. Thibitisha idhini ya usimamizi wa kituo kwa wafanyakazi wa programu na kwa rasilimali zingine zinazohitajika kufanya programu nzuri.

Kuanza 2) Hakikisha mtayarishaji / mwenyeji ana uelewa mzuri wa UVIKO-19 na miongozo ya afya na anaweza kupata habari muhimu zaidi za kurusha hewani. Mtangazaji anapaswa pia kuwa na uwezo uliothibitishwa wa kuwavumilia wasikilizaji, kuwasaidia kuzungumza juu ya wasiwasi wao, kuomboleza hasara yao, kuwasaidia wanapochukua hatua muhimu, na kusherehekea mafanikio yao.

Kuanza 3) Buni programu ya kila siku / ya kila wiki, na ubainishe wafanyakazi, vifaa, na rasilimali zingine zinazohitajika. Unapaswa kuwa na programu ya kila siku au ya kila wiki ambayo ina urefu wa dakika 15-60. Ikiwezekana, tangaza kurudia programu ya kila wiki siku nyingine na wakati mwingine.

Kuanza 4) Tengeneza matangazo ya kila siku (yatakayotangazwa katika mapumziko ya kituo na wakati wa programu zingine) ili kuimarisha ujumbe wa programu kuu ya UVIKO-19.

Kuanza 5) Wasiliana na wakala wa eneo ambalo linaratibu majibu ya UVIKO-19 katika eneo lako. Pata idhini yao ku:

  • Toa tafsiri ya wazi ya miongozo ya kitaifa ya afya katika lugha ya wasikilizaji wako.
  • Toa taarifa za mara kwa mara kuhusu shughuli za UVIKO-19 ambazo wakala hufuata katika eneo lako.
  • Toa habari kuhusu vituo gani vya matibabu vinavyopatikana kwa wasikilizaji ambao wana dalili mbaya, na huduma zipi zinazopatikana kwa watu walio na dalili mbaya. Jifunze juu ya hatua ambazo wasikilizaji wanahitaji kuchukua kuwasiliana na vituo vyao vya matibabu.
  • Toa wataalamu kwa ajili ya mahojiano (kwa njia ya simu au ana kwa ana lakini kwa kukaa umbali wa mita kadhaa).
  • Tangaza programu ya UVIKO-19 ya kituo chako.
  • Toa takwimu za mara kwa mara kuhusu hali ya janga katika eneo lako, kwa mfano:
    • mwenendo wa maambukizi katika eneo lako: visa vinaongezeka? Kupungua?
    • idadi ya watu walioambukizwa, (wazee, walio katika umri wa kati, vijana, watoto)
    • idadi ya watu waliolazwa hospitalini
    • idadi ya watu waliopona
    • idadi ya watu ambao wamekufa
  • Toa habari kuhusu "maeneo maalumu" ya eneo yanayohusika na idadi kubwa ya maambukizo.

Ikiwa mawasiliano yako na wakala wa karibu wa UVIKO-19 hayakupi unachohitaji, wasiliana na wakala wa kitaifa anayeratibu taarifa za kitaifa kuhusu UVIKO-19. Tafuta msaada gani wa kawaida unaweza kupata kutoka kwao (kwa mfano, habari, mahojiano, n.k.)

Inaweza kuwa ngumu kwa vituo vingi vya redio kuratibu kazi hizi na wakala wa eneo husika au wa kitaifa. Katika hali hii, waombe vikundi vya wanawake, vituo vingine vya redio, vituo vya afya, wanasiasa wa eneo husika, na viongozi wa eneo wawasiliane na wakala wa eneo husika au wa kitaifa.

Kuanza 6) Tafuta viongozi wa eneo husika wenye ujuzi ambao wanakubali kuhojiwa mara kwa mara na kushiriki katika majadiliano ya jopo (ikiwezekana) na mahojiano ya mtu mmoja mmoja. Hawa wanapaswa kujumuisha viongozi kutoka:

  • Mashirika ya wanawake
  • Mashirika yanayoongozwa na vijana na vilabu vya shule
  • Mashirika ya wakulima
  • Mawakala wa afya na matibabu
  • Shule na taasisi za mafunzo
  • Vikundi vya wauzaji katika masoko
  • Serikali za jadi na zilizochaguliwa
  • Dini zilizopo katika eneo lako
  • Washauri wenye mafunzo
  • Wengine wanaoonyesha uongozi mzuri katika eneo lako.

Kuanza 7) Tafuta raia wa eneo hilo ambao wamepona UVIKO-19 (au ambao wana wanafamilia ambao wamepona) na wako tayari kuzungumza juu ya uzoefu wao. Hii itasaidia kuleta ukweli wa ugonjwa nyumbani. Pia itasaidia kuvunja unyanyapaa ambao unaelekezwa kwa manusura wengi, na kupingana na hadithi kwamba ukishaambukizwa UVIKO-19, unakuwa nao katika maisha yako yote. Itasaidia pia watu kuwasiliana na kukutana na wale ambao wamepona bila kuwanyanyapaa. Wasiliana na waganga wa jadi ili kuona kama wapo wagonjwa ambao wamekuwa wakiwapa rufaa kwenda kwenye kliniki za kawaida, hospitali, na vituo vya afya, uwahoji hewani, na uulize kwanini.

Kuanza 8) Fikia vituo vingine vya redio vijijini nchini mwako na ujue wanafanya nini na ni maoni gani na rasilimali za programu unazoweza kuwashirikisha. Unaweza pia kutumia rasilimali za FRI kwenye UVIKO-19, inayopatikana hapa.

Kuanza 9) Tafuta njia ya kupata mrejesho kutoka kwa wasikilizaji wako na kutoka kwa mamlaka ya afya ya karibu juu ya jinsi programu yako ya UVIKO-19 inavyofaa. Fanya maboresho ya programu yako kadri unavyoendelea nayo. Kwa mfano, unaweza:

  • Kuruhusu kupokea simu na uulize wasikilizaji wana maoni gani kuhusu programu yako ya sasa ya UVIKO-19 na nini zaidi wanahitaji.
  • Fanya uchaguzi kwa njia ya simu.
  • Kuwa na majadiliano ya jopo na viongozi wa eneo, ukiuliza maoni yao kuhusu programu yako ya UVIKO-19 na nini zaidi wanahitaji.

Kuanza 10) Thibitisha idhini ya wasimamizi wa kituo kuhusu mpango wa kuwaweka wafanyakazi wa kituo na wa programu pamoja na wageni wa kituo salama. (Tazama hapo juu.)

Kuanza 11) Hifadhi maelezo/Maandishi. UVIKO-19 labda sio janga la mwisho ambalo utaliona. Anza na uweke kumbukumbu ya maelezo yanayoelezea masomo uliyojifunza: kwa mfano, nini kinachofanya kazi na kisichofanya kazi, na jinsi unavyoweza kufanya mambo vizuri katika janga la baadaye.

Kiambatanisho 1

Ni wapi tunaweza kupata msaada zaidi kutoka Farm Radio International na vyanzo vingine ili kutengeneza programu inayofaa ya UVIKO-19?

Pata tangulizi za FRI, mwongozo kwa watangazaji unaoonyesha jinsi ya kufanya, Maswali Yanayoulizwa Sana, karatasi za mambo ya ukweli, na vyanzo vingine vya taarifa kuhusu UVIKO-19 hapa. Pata hadithi zetu za Mkulima zinazohusiana na UVIKO-19 (na dharura zingine) hapa.

Chagua orodha ya vyanzo vya taarifa za UVIKO-19:

Kiambatanisho 2

Sampuli ya vipengele vya programu na vitu vinavyoonyesha madhumuni sita ya programu inayofaa ya UVIKO-19

Hapa kuna maoni ya programu ambayo yamejumuisha madhumuni sita ya ufanisi wa UVIKO-19 iliyotajwa hapo juu. Programu zinazofaa za UVIKO-19 zinapaswa kushughulikia kila moja ya madhumuni haya, ingawa vipindi binafsi haviwezi kujumuisha madhumuni yote sita.

1) Toa habari sahihi juu ya hali ya UVIKO-19 katika eneo lako na nchi yako.

  • Toa habari kuhusu maendeleo ya janga katika eneo lako, na majibu yake. Hii inaweza kujumuisha:
    • Ni athari gani za UVIKO-19 kwa wanawake? kwa wakulima? kwa wauzaji?
    • Serikali inafanya nini kupambana na ugonjwa huo katika eneo lako?
    • Kuna athari gani kwa usambazaji wa chakula, kwa lishe, na kwa ajira?
    • Watu wa eneo hili wanazingatia vipi miongozo ya kitaifa ya afya?
  • Serikali imeamuru raia kuchukua hatua maalum?
  • Pata ripoti za simu kutoka vijiji vilivyo mbali, ukionyesha maoni maalum na hatua mazuri wanazochukua huko.
  • Toa matangazo juu ya shughuli zozote za UVIKO-19 zinazokuja katika eneo lako, kwa mfano, tarehe au tarehe zinazokadiriwa kuwa chanjo hiyo itapatikana katika nchi yako, na mpango gani wa kuwapa chanjo wafanyakazi wa afya walio katika mstari wa mbele, watu walio na maswala ya msingi ya kiafya, wazee, nk.
  • Hapa kuna mifano ya mipango ya serikali ambayo inasaidia moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja watu au biashara wakati wa UVIKO:
    • Nchini Rwanda, pamoja na vizuizi vya moja kwa moja mnamo Machi 2020, serikali ilisambaza chakula kwa kaya zilizo hatarini kote nchini na vile vile kupanga bei ya vyakula 17 muhimu, ikiwa ni pamoja na mchele, tambi, unga wa mahindi, maharagwe, sabuni, mafuta ya kupikia, na unga wa uji. Serikali pia ilipanga bei za vyakula vilivyosindikwa, ambavyo vingi vinaingizwa kutoka China.
    • Nchini Kenya, programu zilizopo za uhamishaji wa fedha zinalenga zaidi ya watu milioni, ambao hupokea shilingi 2,000 za Kenya, au $ 19, kwa mwezi. Serikali ilitenga ziada ya shilingi bilioni 10 kwa mpango huu kusaidia vikundi vilivyo hatarini pamoja na wazee na yatima wakati wa janga hilo.
    • Nchini Burkina Faso, mpango mpya wa uhamisho wa pesa milioni 10 kwa wauzaji wa matunda na mboga ulitangazwa.

2) Sahihisha habari za kughushi na habari potofu

Sahihisha habari yoyote ya uwongo na habari za kughushi zinazoenea katika eneo lako. Ruhusu kupigiwa simu na uulize wasikilizaji wazungumze juu ya habari yoyote ya tuhuma au madai juu ya UVIKO-19 na jinsi ya kukabiliana nayo. Hakikisha una mgeni ambaye anaweza kushughulikia habari hii. Kuna idadi kubwa ya habari za kughushi, uwongo, na hadithi zinazozunguka juu ya mambo mbalimbali ya janga la UVIKO-19, kwa mfano, tiba za kuponya ambazo hazina uthibitisho (tiba ya mvuke, joto, baridi, vitunguu, tangawizi, nk) au kupendekeza kuwa janga hilo yenyewe au chanjo mbalimbali ni sehemu ya njama za kisiasa.

Kwa habari zaidi juu ya kutambua na kupambana na habari za kughushi na upotoshaji, angalia habari za kughushi: Jinsi ya kuitambua na nini cha kufanya juu yake https://africacheck.org/2020/12/14/fighting-the-UVIKO-19-infodemic-five-strategies-for-african-fact-checkers

3) Tangaza na ufafanue miongozo ya afya mara kwa mara, kwa lugha ya wasikilizaji wako.

  • Hakikisha kitengo cha afya cha eneo lako kinatoa tafsiri ya wazi ya miongozo ya kitaifa ya afya katika lugha ya wasikilizaji wako.
  • Unda neno moja au zaidi la uhamasishaji na lakukumbukwa ambayo linashughulikia miongozo yote mikuu, litangaze ndani ya programu yako ya UVIKO-19 na wakati wa mapumziko ya kituo. Unaweza kurusha safu mbili za matangazo za FRI kuhusu UVIKO-19. Zipate hapa na hapa.
  • Tangaza miongozo ya afya ya UVIKO-19 kwa siku zote saba za ratiba yako ya programu ya kila wiki.
  • Rusha mahojiano mepesi na watoto na wengine ambapo wanajaribu kusoma miongozo hiyo — na kukosea baadhi yao! Hakikisha unafanya marekebisho kwa upole!
  • Waombe wasikilizaji watunge mashairi, vitendawili, au nyimbo kuhusu miongozo hiyo.

Endesha jaribio, aidha iwe ni kwa njia ya simu au mubashara ndani ya studio (kwa kuzingatia kukaa kwa umbali unaofaa na kufuata hatua zingine za kinga). Jaribio lizingatie juu ya njia ambazo ugonjwa huenezwa, hadithi za uwongo na habari potofu, ukweli juu ya chanjo, n.k. Jaribio linapaswa kuchanganya habari na burudani, na lazima lijumuishe mtaalam anayeweza kuzungumza kwa mamlaka, kuondoa hadithi za uwongo na kusema ukweli.

4) Wape viongozi wa eneo husika nafasi ya kuonyesha uongozi katika juhudi za kusaidia kuzuia kuenea kwa UVIKO-19.

Hii inaweza kujumuisha:

  • kuelezea namna wanavyounga mkono miongozo ya afya
  • kuelezea jinsi miongozo itakavyotekelezwa katika umoja wao
  • kuelezea maoni yoyote walio nayo juu ya kutekeleza miongozo, na jinsi watakavyoshughulikia maswala haya.

5) Wape wasikilizaji nafasi ya kusema kuhusu maoni yao juu ya kufuata miongozo-na kuhakikisha maoni yao yanashughulikiwa na maafisa wenye ujuzi, wataalam wa afya, na wasikilizaji wengine.

Wakati wa mafadhaiko makubwa, mara nyingi watu huwageukia viongozi wa eneo wanaoheshimiwa kwa ajili ya kupata huruma, mwongozo, msaada, na mfano. Unapaswa kuhoji viongozi wa eneo ambao ni viongozi wa jadi, maafisa wa raia, maafisa wa afya wa eneo hilo, wakuu wa mashirika ya wakulima na wanawake, viongozi wa dini, waalimu, nk.

  • Kuwa na muda wakati wa kipindi abapo wasikilizaji watapiga simu na kuelezea maoni au wasiwasi wao.
  • Kuwa na mgeni mwenye ujuzi ambaye anaweza kushughulikia maoni au wasiwasi wa wasikilizaji.
  • Ikiwa vinapatikana, tangaza vipindi vya mchezo wa kuigiza ambao unaigiza maisha ya familia inayoishi na changamoto za UVIKO-19.

6) Saidia wasikilizaji na mashirika wanapofanya kazi kushinda changamoto na kupitisha miongozo ya afya.

  • Anza programu na sauti ya kiashiria (kiashiria) "kwa pamoja tunaweza kulishinda hili” ujumbe.
  • Mwenyeji afanye mtazamo mzuri kwa ujumla wakati wote wa programu, wakati akikubali hitaji la utatuzi wakati wa kuhojiana na mtu ambaye amepata hasara.
  • Fanya mahojiano na watu wa eneo hilo ambao wamechukua hatua muhimu kusaidia jamii kufuata miongozo hiyo, mfano.
    • Kuanzisha semina ya kutengeneza barakoa.
    • Kuanzisha biashara ya kutengeneza sabuni.
    • Kutengeneza mazingira ya kukaa kwa kuachiana nafasi kwenye soko ili kulinda afya ya wachuuzi na wanunuzi na watu wengine kama hao.
    • Kuwafanya wanaume kushiriki utunzaji wa familia na majukumu mengine ya nyumbani na jamii.
  • Toa nambari ya simu ambayo wananchi wanaweza kupiga simu kuelezea shida wanayoipata kupitisha mwongozo mmoja au zaidi. Kuwa na mtu mwenye ujuzi atoe ajibu na jibu liwe lenye kusaidia. Tangaza maswali ya simu na majibu hewani.
  • Acha raia watumie nambari ya simu kushirikisha vidokezo juu ya jinsi wanavyotumia mwongozo mmoja au zaidi katika hali ngumu. Toa tuzo ya kila wiki kwa mtu aliye na kidokezo bora.
  • Tuma salamu kwa mtu yeyote anayesafiri kwenda eneo lako kwa kazi ya kukabiliana na UVIKO-19. Wahoji hewani ikiwa unaweza.
  • Maliza programu na promo nzuri kwa kipindi kijacho.
  • Panga "siku" maalum au hafla za programu ambapo unasherehekea mafanikio mbalimbali ya UVIKO-19, kama vile:
    • Kupunguzwa kwa idadi ya kesi mpya za maambukizi zilizoripotiwa na maafisa wa afya.
    • Ufunguzi wa kikundi kipya cha kutengeneza barakoa.
  • Wahoji watu wa eneo hili ambao wanachukua hatua nzuri ya kujiweka sawa na kusaidia wengine kuwa na afya.
  • Mhoji na mtu aliyeambukizwa ambaye alitibiwa UVIKO-19 na alipata matibabu muhimu.
  • Fanya mazungumzo ya kawaida kwa njia ya simu ambayo yanahimiza wasikilizaji kutoa wasiwasi wao, na hiyo inaruhusu wataalam na wasikilizaji wengine kuelezea jinsi ya kushinda wasiwasi huo.
  • Ikiwezekana, kuwa na sehemu ya "piga kuchagua" ambapo wasikilizaji wanaweza kupiga kura kwa njia ya simu juu ya changamoto zipi muhimu zaidi wanazokabiliana nazo wakati wa kutekeleza miongozo hiyo. Kuwa na mtu mwenye ujuzi ajibu matokeo ya kura.
  • Maliza na promo ya programu yako inayofuata na muhtasari wa yaliyomo ya muhimu zaidi.
  • Sherehekea mafanikio ya raia na mashirika katika kutekeleza miongozo ya kitaifa ya afya.
  • Fupisha muhtasari wa mambo muhimu ambayo wasikilizaji wanapaswa kukumbuka kutoka kwenye kipindi hiki.
  • Asante wasikilizaji na wote ambao wanaweka mpango pamoja, na toa ujumbe wa kufunga wa matumaini na msaada.
  • Cheza wimbo wa kiashiria ambao unatia nguvu na wenye kuonyesha matumaini "ikiwa sote tunafanya kazi pamoja."

Kiambatanisho 3

Sampuli za karatasi za kuendesha kipindi cha programu ya UVIKO-19

Sampuli 1

Sampuli 2

 

Shukrani

Imechangiwa na: Doug Ward, Mwenyekiti wa zamani, Farm Radio International.