Mifumo ya muingiliano kuwatia moyo wasikilizaji kushiriki

Programu ya muingiliano ni nini?

Programu za muingiliano ni zile zinazohusisha au kuvutia mawasiliano ya pande mbili kati ya kituo cha redio na wasikilizaji wake. Mawasiliano hayo yanaweza kuwa ya ana kwa ana, kupitia simu, ujumbe wa maandishi au barua au inaweza kuwa kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook na njia zingine za mawasiliano mitandaoni. Mawasiliano hayo ya pande mbili yanaweza kuwa kati ya msikilizaji na mtangazaji, msikilizaji na mwanasiasa, msikilizaji na wakala wa uenezaji, msikilizaji na mwakilishi wa shirika lisilo la kiserikali au kati ya wasikilizaji wawili au zaidi. Programu za muingiliano zinaweza kurekodiwa studio au shambani na zinaweza kuwa mazungumzo yanayohusisha watu wawili au zaidi.

Mawasiliano ya muingiliano yanawaruhusu watazamaji kutoa maoni yao na sauti zao zisikike redioni na katika jumuia yote. Inasaidia kuhakikisha kwamba ujumbe uliomo katika programu za redio unaongozwa na mahitaji ya jumuia na sauti za jumuia. Faida moja kubwa sana kwa kituo cha redio ni kwamba, wanayo fursa ya kupata maoni yahusuyo mambo yaliyo muhimu katika jumuia. Kwa kusimamia programu ya muingiliano, kituo kinaweza kujua zaidi mahitaji ya wasikilizaji wake.

Programu za muingiliano zinazowapa wasikilizaji fursa ya kusikia sauti zao hewani huwa ni kati ya vipindi maarufu sana vya redio. Programu za kupiga simu na kutuma ujumbe wa maandishi ni maarufu kwanza kwa sababu watu hupenda kusikia sauti zao wenyewe na watu kama wao wakiongea. Wote huwa tuna udadisi wa kutaka kujua watu wengine wanafikiri nini na wanahisi nini.

Ila shaka vipindi vya majadiliano si njia pekee za kuhusisha hadhira. Aina nyingine za programu pia ni za muingiliano zikiwemo kuomba kupigiwa muziki, matangazo ya bure ya biashara, mashindano ya redioni, michezo, mashindano ya vipaji, vivutio na vipindi vya maswali na majibu. Maoni ya watu, matangazo sehemu ya tukio na majadiliano kati ya jopo la watu yanaweza kufaa kuwa programu za muingiliano.

Programu za muingiliano ni za ushiriki kwa sababu zinawawezesha wasikilizaji kutaja matatizo yao na kuamua wenyewe kuhusu malengo yao, katika mchakato wa kufanya maamuzi yao. Programu za muingiliano zinaweza kuwa mabaraza ya kutoa malalamiko yao na matumaini yao, ya kushangilia mafanikio ya jumuia na ya kushughulikia masuala mazito

Kwa mfano, mtayarishaji wa kipindi anaweza kutambulisha jambo ambalo linawasumbua wengi katika jumuia, halafu aorodheshe malalamiko na madai yao majumbani kwao na maeneo yao ya kazi. Masuala hayo yaliyorekodiwa yanachezwa na meya na mamlaka husika wanasikiliza. Malalamiko ya watu na majibu ya mtawala yanatangazwa katika kipindi kinachoyatoa yote kwa pamoja na wasikilizaji wanakaribishwa kupiga simu na kutuma ujumbe wa maandishi.

Programu nyingine inaweza kuwa ni kurekodi kikundi cha wasikilizaji wa redio ambacho kinaelezea maoni yao wenyewe kuhusu programu Fulani. Kwa mfano, kuanzia mwaka 1998-2001 kulikuwa na ubia kati ya Panos, shirika la Utangaji la kitaifa na vikundi kumi na tatu vya wasikilizaji vya kinamama. Vikundi hivyo vilikutana kila wiki kusikiliza makala za redio na kujadiliana masuala ya maendeleo. Walirekodi majadiliano yao, halafu wakayapeleka kwa mtayarishaji. Mtayarishaji anamwendea ofisa mhusika, anayeombwa kujibu masuala yaliyoletwa katika mjadala na kikundi hicho kwa kutoa taarifa, na ikiwezekana, kwa kuweka ahadi ya kuyafanyia utendaji. Mjadiliano hayo na majibu hayo yalirekodiwa pamoja na kurushwa kila wiki ili vikundi hivyo visikilize na kujadiliana. Mtayarishaji anafuatilia mtoa majibu na vikundi hivyo ili kuhakikisha kwamba ahadi hizo zilikuwa zikitimizwa na vikundi hivyo kutumia nyenzo zilizoahidiwa.

Swali moja kubwa
Sawa, unaweza kusema, programu za muingiliano zinaonyesha zinafaa sana. Lakini kwa mfano, vipindi vya kupiga simu vinafanikisha lolote zaidi ya mjadala mkubwa wa wazi? Je, inaweza kufanikisha chochote?

Mara nyingi inafanikisha. Mfano mmoja ni huu. Septemba, 2010, ujumbe wa maandishi uliotumwa kwenye kipindi cha asubuhi katika redio ya Joy FM mjini Accra, Ghana ulileta suala la kuzagaa kwa nzi weusi katika chanzo cha maji ya kunywa kwenye jumuia ya vijijini. Mwanabaraza wa hapo alijaribu kulielezea suala hilo kwa mamlaka ya afya bila ya mafanikio. Majadiliano ya wazi na ufuatiliaji wa makini wa Joy FM hatimaye ulifanya tatizo hilo kushughulikiwa kwa kuwapima na kuwatibu wale walioathirika na tatizohilo, na jumuia ikapewa maji ya kunywa. (Tazama:http://edition.myjoyonline.com/pages/news/201012/57189.php)

Mojawapo ya njia ya mafanikio haya ni ukweli kwamba JOY FM imejenga kuaminiwa na imekubalika na wasikilizaji wake, na imeendeleza mahusiano mazuri kwa kipindi kirefu na watawala wa miji. Msisitizo na uadilifu wa kipindi kirefu wa kituo hicho ukasababisha ….matokeo!

Jinsi muingiliano unavyoonekana: Mifumo ya redio yenye muingiliano
Kuna sababu nyingi za kwa nini vituo vya redio vinatangaza programu za muingiliano, na kuna aina nyingi za programu za muingiliano. Aina hizo ni kama vile: Kupiga simu kituoni, kutuma ujumbe wa maandishi, kuandika barua.

 • Majadiliano ya jopo- kituoni au mahali pa tukio.
 • Mikutano ya ukumbi wa mji.
 • Matangazo kwenye tukio.

Baadhi ya njia za kutayarisha programu za muingiliano ni hizi:

Kumualika wakala wa uenezaji au mtaalamu anayehusika na suala linalozungumziwa na wasikilizaji wapige simu kuhusiana na suala linalijadiliwa.

 • Kumualika mwanasiasa wa eneo hilo, wa mkoa au wa kitaifa ili aelezee au atoe maelezo kuhusu sera za serikali.
 • <

 • Kuwa na jopo la majadiliano juu ya mada za kilimo.
 • <

 • Kuwapa kikundi cha wasikilizaji kifaa cha kurekodia na warekodi maoni yao kuhusu.

Programu Fulani au suala Fulani la jumuia. Maoni hayo yarushwe hewani. (Hii inaweza kusaidia kukionyesha kituo vipaumbele, mahitaji na mambo yanayopendelewa na jumuia.)

Programu nane za muingiliano

Mifano nane ifuatayo inaonyesha kwa nini vituo vya redio na mashirika ya maendeleo yanaandaa programu za muingiliano, na manufaa kadhaa ya programu za muingiliano.

1. Mega FM (Gulu, Uganda)

Jina la programu: Kabake

Sababu za kuanzisha programu hiyo:Kukuza mijadala ya wazi juu ya masuala yanayoathiri jumuia za maeneo ya kaskazini mwa Uganda, ikiwemo makazi mapya na maendeleo ya kijamii na kisiasa.
Kuboresha maisha ya wanyonge kwa kutambulisha na kujadili kuhusu mahitaji na utatuzi wa mahitaji ya eneo Fulani.
Kutia moyo muingiliano na kuishi pamoja kwa amani kati ya watu waliokuwa katika makambi ya wakimbizi wa ndani.

Mfumo: Midahalo iliyorekodiwa kabla huko vijijini.

Aina ya muingiliano: Midahalo katika eneo husika

Maelezo: Katika lugha ya Acholi, Kabake inaelezewa kama baraza ambalo wanajumuia wanakutana na kujadili matatizo yao na kupata suluhisho la pamoja. Kabake inawapa raia wa mijini na vijijini fursa ya kujadili mada za kisiasa na kijamii katika kikundi. Timu ya wasimamizi na maofisa wa kiufundi wanasafiri kwenda hata kwenye jumuia za mbali ili kurekodi midahalo. Makala hizo zimekuwa zikitangazwa kwa dakika 90 kuanzia mwaka 2003.

Matokeo: Tathmini ya 2010 ilionyesha kwamba kipindi hicho kina umarufu sana. Viongozi wa vijiji wanachukulia kwa umakini malalamiko yanayozungumziwa katika programu hiyo. Kabake imeisaidia jumuia kuwawajibisha viongozi wa vijiji na wa kiserikali. Kupitia midahalo hiyo na matangazo, jumuia zimejipanga kujishughulisha na miradi, ikiwemo makazi mapya na kuishi pamoja kwa amani. Midahalo hiyo inasemekana kuziba pengo lililokuwepo katika mawasiliano na uwajibikaji unaohusiana na serikali na demokrasia katika jimbo hilo.

Kwa taarifa zaidi: Konrad Adenaeur Stiftung: Kabake! Redio yenye muingiliano katika kiwango cha wananchi wa kawaida nchini Uganda. http://www.kas.de/uganda/en/publications/23197/

2. CBS (Kampala, Uganda)

Jina la programu: Nekolera Gyange (Naendesha biashara yangu mwenyewe)

Sababu za kuanzisha programu: Kuwapatia wafanyabiashara wadogo (wenye biashara ndogondogo, kwa kawaida waliojiajiri na kwa sehemu ya ‘uchumi usio rasmi’) sauti ya kuweka ushawishi katika mazingira yao ya kazi na maamuzi ya sera, jukwaa la majadiliano na njia ya kupokea taarifa muhimu ili biashara zao ziendelee.

Mfumo: Mfumo wa gazeti hilo ni pamoja na habari za kibiashara, vipindi vya majadiliano, mahojiano na wenye biashara ndogondogo, wataalamu na watengenezaji wa sera; na kupiga simu wakati kipindi kikiendelea. Asilimia sabini hadi themanini ya muda wote wa makala hiyo unawashirikisha wasikilizaji katika mahojiano, mazungumzo na aina nyingine za muingiliano. Kuna mashindano ya kukuza maendeleo ya biashara, fursa za kibiashara kwa watu wanaotaka kununua kutoka kwenye biashara ndogondogo kutangaza zabuni zao bila malipo, na ufuatiliaji wa waandaaji wa programu juu ya malalamiko yaliyopokelewa na wenye biashara ndogondogo.

Aina ya muingiliano: Kupiga simu.

Maelezo: Ilitangazwa kwa mara ya kwanza Oktoba, 1999. Programu ya mlengo ya Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO ya kuongeza Ajira kupitia Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo (SEED), inatoa msaada wa kiufundi kwa CBS kwa kuanzisha programu zenye msingi wa kibiashara, Kwa hiyo kuhakikisha kwamba programu hizo zinakua na kuendelea bila mafungu ya fedha ya umma. Watumishi wa Programu hiyo wanafanya utafiti wa suala Fulani kwa mbinu ya uandishi wa kipelelezi, halafu wanawahoji wamiliki wa biashara ndogondogo, wataalamu wa kiufundi na watawala wa serikali waliopo. Mahojiano hayo yanahaririwa na kuchanganywa na masimulizi ya mtangazaji ili kupata makala kamili. Kwa kawaida, makala zinachanganywa na kipindi cha mahojiano ya moja kwa moja ikihusisha wawakilishi kutoka makundi yote matatu. Halafu, watumishi wanaandaa jinsi ya kupokea matokeo, labda kwa simu wakati wa kipindi cha kutoa maoni au miito, ujumbe wa maandishi na ujumbe wa faksi baada ya kipindi. Mwishoni, timu inafuatilia masuala hayo ya programu ili kuona mabadiliko yanayokuwa yametokea. Namna hii ya makala inachukua vipindi kadhaa. Tathmini ya programu inaonyesha kwamba asilimia 40 ya wajasiriamali wadogo na wa kati ni wasikilizaji wa kilia wakati. Biashara tisa kati ya kumi zilizoonyeshwa zilipata faida kwa kuwa katika programu hiyo. Nusu ya biashara zilizoonyeshwa ziliongeza mauzo na mbili kati ya hizo (asilimia 20) ziliongeza wafanyakazi wawili zaidi. Waandaaji sera watano kati ya sita waliojitokeza katika programu waliripoti kwamba mtazamo wao na sera zao zilibadilika kutokana na programu hiyo. Mmoja alisema alipokea simu nyingi baada ya kusikika redioni, wakilalamika kuhusu watoza ushuru wakiwanyanyas sana. Mtawala huyo alilipeleka suala hilo kwa Mamlaka ya Kodi ya Uganda na unyanyasaji huo ukakoma. Ushahidi wa ubora unaonyesha kwamba athari kubwa kabisa za programu hiyo ni pamoja na:

 • Kuonyesha umuhimu wa sekta ya wajasiriamali wadogo kibiashara, kiuchumi na kisiasa kwa watangazaji wa biashara na watengenezaji wa sera.
 • Kuwapatia wajasiriamali wadogo sauti ya umma na kuwaunganisha na mfumo wa maendeleo wa kisiasa, na hivyo kuchangia katika jamii ya kiraia na kidemokrasia ya Uganda.
 • Kuonyesha kwamba programu za magazeti pamoja na mifumo ya
  muingiliano vinaweza.

Kwa maelezo zaidi: Shirika la kazi duniani, 2002. Mapinduzi ya Taarifa kwa Ujasiriamali wa Africa: Ujuzi katika mifumo ya mifumo ya muingilianokwa redio.. Tazama katika http://www.ilo.org/empent/Publications/WCMS_117709/lang–en/index.htm

Radio Mang'elete (Kenya)

Jina la programu: Wanawake na maendeleo, na kushirikishana keki

Sababu za kuanzisha mradi: Kuwasaidia wanawake wa vijijini kuelezea mahitaji yao, maoni na ujuzi wao. Kuongeza hadhi na kujihusisha kwa wanawake katika redio ya jumuia, na kuwapa wasikilizaji wa redio na hasa wanawake, sauti ya kuwa na mwitikio kwa programu na kushiriki katika uundaji wa maudhui ya programu.

Mfumo: Wanawake na maendeleo inahusisha mahojiano na wanawake walio katika vikundi vya wanawake, na mahojiano na wanawake wengine- kwa mfano, programu juu ya haki za kimila na kisheria za wanawake iliwahoji wanawake wanaofanya kazi kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshughulikia masuala ya jinsia au waliokuwa wakigombea uongozi wa serikali za mitaa. Shiriki Keki ni programu ya midahalo ya kijumuia.

Aina ya muingiliano: Wanawake wanatoa maoni yao kituoni juu ya mada wanazozipendelea kupitia chombo hicho cha hewani (tazama hapo chini). Maneno yao yanatolewa katika programu zote mbili.

Maelezo: Ikiwa sehemu ya mradi wa utafiti wa chuo kikuu uliofadhiliwa kwa sehemu na Microsoft, wanawake walio katika vikundi vya mitaani walipewa chombo cha kushikilia mkononi kurekodi sauti za maoni yao kwa teknolojia iitwayo maendeleo kupitia redio ya.

(Kifaa hicho kilitengenezwa kisifanane na simu ya mkononi kwa sababu wanawake walisema kuwa kinaweza kuchuliwa na waume zao na kuuzwa). Vikundi hivyo vya wanawake vilitengeneza maudhui kwa ajili ya utangazaji, ikiwemo mahojiano ya vikundi, michezo ya redio, mazungumzo yaliyoongozwa na kikundi hicho na mdahalo. Michezo ya redio ililenga masuala kama ulevi, unyanyasaji wa wanawake, usumamizi wa fedha na elimu ya kienyeji waliyonayo baadhi ya vikundi vya wanawake, kama vile upandaji wa miti na ufugaji wa nyuki. Mada nyingine ni kama mafanikio ya vikundi vya wanawake, wajibu wa kila jinsia, kanisa, VVU na UKIMWI, haki za wanawake, elimu, haki za kumiliki ardhi, jinsi ya kuwatendea wajane, ubaguzi jinsia na utamaduni. Masuala ambayo wanawake hao waliyajadili katika programu ya Wanawake na maendeleo yalipelekea kuundwa kwa programu ya mdahalo wa redio unaoitwa Kushirikiana Keki, ambapo wanawake na wanaume wanajadiliana mada zinazohusu maeneo yao. Tukio moja lilijadili juu ya sifa za adhabu za kimila katika uaminifu kwenye ndoa. Tukio jingine lilijadili suala la vijana wa kiume kushiriki ngono na kinamama wakubwa zaidi yao.

Matokeo: Tathmini ya matokeo ilikuta kwamba redio hiyo iliyoongezewa nguvu na AIR- inatoa njia ya kuyaweka wazi matatizo ya wanawake na kufanya sauti zao ‘zisikike’ na wanaume, amabayo imebadilisha mahusiano ya jinsia hizo mbili ndani ya jumuia. Mradi huo umeonyesha kwamba wanawake wako radhi kujadili masuala kama vile VVU na UKIMWI, ukahaba, uchawi, uhamiaji na elimu na wanachangamka katika kupaza sauti zao na majina yao hewani, kwa upande mmoja ni kwa sababu wanaona redio ya jumuia kama ‘mahali pa maendeleo. Programu juu ya taarifa za afya na uzuiaji wa ukatili majumbani zimepelekea mabadiliko katika jumuia, kama vile programu iliyotoa taarifa juu ya tishio la mahindi yaliyotiwa sumu ambalo lilikuwepo kwa sababu ya matangazo juu ya hatari iliyokuwepo. Programu zote mbili za midahalo zinazotangazwa zimepekea kupata miito zaidi ya hamsini, jumbe za maandishi na barua kadhaa kuja kituoni. Wanawake na wanaume vijana kwa wakubwa walishiriki.

Kwa taarifa zaidi: S. Revi Sterling. Maendeleo kupitia muingiliano redioni. Kuwasilisha kwa picha. http://research.microsoft.com/en-us/events/indiasummerschool2010/sterling-msri_air.pdf
Revi Sterling, 2010. 89.1FM: Mahali pa maendeleo: Kuhamisha nguvu na nafasi ya ushiriki katika ICTD. Jarida la Habari za Jumuia. Kitabu cha 6, No. 1, 2010. http://ci-journal.net/index.php/ciej/article/view/637/461

4. Redio DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati

Jina la programu: Redio ya muingiliano kwa ajili ya mradi wa Sheria ulijumuisha programu zifuatazo:
Redio ya muingiliano ya mfululizo wa vipindi vya haki
Kujadiliana kuhusu haki
Mtoto: Hapo mwanzo akiwa porini, Leo akiwa sehemu ya jumuia
Mapatano yetu
Mjadala wetu Kuhusu Amani na Haki
Njia ya kulekea kwenye haki

Sababu za kuanzisha programu hii: Kutia moyo mazungumzo kati ya watu na mamlaka za kitaifa/kimataifa katika maeneo ambayo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inapeleleza uhalifu kama mauaji ya kimbari na makosa ya kivita. Wawakilishi wa mamlaka hizi wanaoshiriki katika mazungumzo hayo ni wale wanaowajibika kwa maamuzi ya kisheria juu ya masuala haya.

Mfumo: Redio ya muingiliano ya mfululizo wa vipindi vya haki ni programu ambayo wasaili wanawauliza maofisa wa ICC maswali yaliyoulizwa na wasikilizaji. Kujadiliana kuhusu haki inaalika maofisa wa kitaifa na wa kimataifa, viongozi wa serikali za mitaa na wanachama wa jumuia za kiraia kwenda kituoni kujadili maswali yaliyoulizwa na wasikilizaji wengi. Katika Mjadala wetu kuhusu Amani na Haki, mamlaka ya kimataifa ya haki inazungumza na viongozi wa jumuia katika maeneo ambayo upelelezi wa kimataifa wa jinai unafanyika.

Aina ya muingiliano: Kujibu maswali ya wasikilizaji; jopo la majadiliano.

Matokeo: Tathmini ya mwaka 2011 ilikuta kwamba uwezo mkubwa wa mradi ulikuwa katika kubadilisha elimu na imani za wasikilizaji wake. Kwa mfano, wasikilizaji walionyesha kupanuka kwa uelewa wa ICC na mamlaka za kisheria na za kitaifa pamoja na wajibu wao. Pia, idadi kubwa ya wanajumuia waliamini kwamba maofisa wa ICC na mamlaka za kitaifa zinaelewa mahitaji yao. Idadi kubwa sana ya makundi ya wasikilizaji iliripoti kuongezeka kwa kutambua uwezo wao kuweza kuleta mabadiliko mazuri. Mradi huo ulionyesha maendeleo katika kuunganisha sauti na maoni ya watu wa aina mbalimbali kwa kuwatia moyo kuzungumza na kuelewa kwamba maoni yao na maswali yao yanathaminiwa.

Kwa maelezo zaidi: Redio ya muingiliano kwa ajili ya haki. http://www.irfj.org/

5. Mishapi Voice TV, Radio Maendeleo, RTG2, Contact FM, Radio Salus, Radio Isanganiro (Redios ya DRC, Rwanda, Burundi)

Jina la programu: Kizazi cha Maziwa Makuu

Sababu za kuanzisha programu: Kilianzishwa katika kutafuta uelewano mmoja, Kizazi cha Maziwa Makuu (Génération Grands Lacs) ilibuniwa ili kutoa nafasi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Rwanda, Burundi na Kongo DRC ili kuwasiliana, kuziba pengo linalowatenganisha, na kuleta jumbe za amani katika hali za misukosuko na vurugu kama zile zinazoendelea Mashariki ya Kongo DRC na kwenye eneo la Maziwa Makuu.

Mfumo: Kipindi cha dakika sitini cha kuongea kwa simu moja kwa moja cha vijana kinarekodiwa moja kwa moja kila jumamosi. Programu hiyo inajumuisha wageni walioalikwa studio, mahojiano yaliyorekodiwa kabla, maoni ya watu, muziki na wasikilizaji wakishiriki kupitia simu, ujumbe wa mtandao, ujumbe wa maandishi na mtandao wa kijamii (Facebook). Vijana wanapiga simu, wanajadiliana na wanashirikishana maoni.

Aina ya muingiliano: Kupiga simu, kutuma ujumbe wa maandishi, ujumbe wa mtandao, mtandao wa kiamii (Facebook).

Maelezo: Kila wiki, toleo la Kizazi Cha Maziwa Makuu linazunguka kwa kupokezana kati ya Kongo DRC, Rwanda na Burundi na kati ya timu ya waandishi wa habari kutoka kwenye eneo hilo. Programu hiiyo inatoa fursa kwa vijana kuongea, kusikiliza na kujifunzakuhusu masuala na changamoto zinazowakabili katika kanda yao. Masuala yanayoshughulikiwa ni pamoja na jinsia, vurugu, utambulisho, ushiriki wa vijana katika siasa na masuala ya ukabila na utaifa.

Matokeo: Kuna usikilizaji wa hali ya juu kati ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Rwanda, Burundi na Kongo DRC, na kipindi kinawafikia vijana wasio wa vyuo vikuu kwa asilimia 30-60. Tathmini ya matokeo imeonyesha: uwiano mkubwa kati ya usikilizaji na kupungua kwa chuki na kupata mtazamo mzuri; Programu hiyo inapelekea ustahimilivu nakupungua kwa mtazamo mbaya; Programu hiyo inawawezesha vijana kushughulikia migogoro kwa namna yenye manufaa. Tathmini ilieleza kwamba pamoja na hali ya hivi karibuni ya kuibuka tena kwa vurugu katika kanda hiyo, kipindi hicho kina wajibu muhimu wa kusambaza ujumbe wa amani na kustamhimiliana na kutoa nafasi ya kufanya mazungumzo.

Kwa maelezo zaidi: Redio jenga amani Africa. Kizazi cha maziwa makuu: Kutumia vyombo vya habari kuziba tofauti na kupata muafaka. http://www.radiopeaceafrica.org/index.cfm?lang=en&context_id=22&context=features&action=oneFeature&feature_id=1
Kutafuta muafaka. Kizazi cha Maziwa Makuu. Mazungumzo ya kila wiki ya Amani, Moja kwa moja redioni. http://www.sfcg.org/programmes/drcongo/pdf/generation_grands_lacs.pdf

6. Shirika la Utangazaji la Malawi Radio One (Malawi)

Jina la Programu: Kanthu n’khama

Sababu za kuianzisha programu: Kukuza mjadala wa kitaifa kuhusu masuala ya maendeleo.

Mfumo: Programu ya gazeti ya dakika 30 inayotangazwa kila jumamosi saa nane mchana.

Aina ya muingiliano: Vikundi vya kusikiliza redio vina andaa programu inayotokana na matatizo yao (kinachoitwa ‘sauti ya kijiji’), halafu wanajadiliana na mtoa huduma anayehusika (‘mjadala’), na kupata programu inayotokana na sauti ya kijiji na mazungumzo yao.

Maelezo: Kanthu n’khama ina dakika tano za mapitio ya kipindi cha wiki iliyotangulia awali, ikifuatiwa na dakika kumi za sauti ya kijiji kutoka katika jumuia hizo, dondoo za michezo ya kuigiza ikiigizwa na vikundi vya wasikilizaji, halafu dakika za muitikio kutoka kwa watoa huduma.

Kuandaa Kanthu n’khama inajumuisha hatua mbili: Kwanza, Vikundi vya kusikiliza redio (RLC) vinarekodi majadiliano ambayo wanaainisha tatizo walilonalo na kutafuta namna wanayofikiri linaweza kutatuliwa. Aina hii ya kurekodi inaitwa mawu (sauti ya kijiji). Sauti za vijiji zinaelezewa kupitia michezo ya kuigiza, nyimbo za kitamaduni, ushairi na majadiliano. Pili, sauti ya kijiji inapelekwa kwa mtoa huduma ambaye anasikiliza ujumbe huo uliorekodiwa na anaandaa majadiliano na jumuia juu ya suala lililoibuliwa. Mjadala wa pili – kati ya RLC na mtoa huduma – unarekodiwa kama ‘mazungumzo.’ Inapofikia mwisho wa mazungumzo, mpango kazi umeshaandaliwa na majukumu ya kikundi cha wasikilizaji na mtoa huduma yanatolewa wazi. Mjadala unarekodiwa na kusimamiwa zaidi na wanachama wa kikundi cha wasikilizaji. Mtayarishaj wa MBC anafanya mapitio ya programu hiyo kiufundi, anaandika maelezo yake, anasikiliza sauti na kuchanganya vipande vya programu. Mijadala inafanyika kati ya RLC na waandaaji wa sera na wahusika. Watoa huduma ni pamoja na sekta ya umma, binafsi na mashirika ya kiraia.

Matokeo: Programu imewezesha jumuia kuwaita maofisa wa ngazi za juu wa umma kama vile mawaziri, kwenda hapo kijijini kuelezea kuhusu maamuzi au huduma zinazotolewa na wizara zao. Katika wilaya ya Mulanje, kwa mfano, Ofisa msaidizi mchunguzi katika wizara ya Afya aliombwa aondoke katika jingo ambalo jumuia lilikuwa limejenga kwa ajili ya Kliniki ya watoto chini ya miaka mitano, lakini ambalo mtumishi huyo alikuwa akilitumia kama makazi ya muda kwa miaka miwili baada ya nyumba yake kupelekwa na mafuriko. Ofisa huyo hakujali kutafuta makazi yake mwenyewe. Jumuia ilimwita ofisa huyo na kudai aliwalipe kodi na kiporo cha fedha kwa sababu amekuwa akichukua posho yake ya nyumba ingawa hakuwa akilipia nyumba.

Hii ikiwa imetengenezwa katika tukio, Kanthu n’khama inakuza hali ya umiliki wa kituo kitaifa kwa kuzipa jumuia uwezo wa kupima maudhui ya program. Siku na wakati wa kukitangaza ulichaguliwa na wanajumuia wenyewe.

Kwa maelezo zaidi: Linje Manyozo, 2007 Mbinu na utendaji katika ushiriki wa redio. Ecquid Novi: Masomo ya uandishi wa habari Afrika, 28 (1 & 2): 11-29.
Susan Sisya, Kampeni ya mabadiliko ya kijamii kupitia Kanthu-N’khama. http://www.freewebs.com/linjem/kuchezanewsletter.htm

7. Sanyu Fm, Radio Wa, Radio Pacis (Arua), Savoir FM, Delta FM, Radio Pacis (Gulu) (Uganda)

Jina la Programu: Vipindi kadhaa vya majadiliano vilivyoongezewa nguvu na kifaa maalum.

Sababu ya kuanzisha program: Kuzihusisha jumuia za mitaani ili kuripoti matatizo kwenye huduma za umma na kuwapatia jukwaa la kushiriki na kujadili masuala ya sera. Kukuza uwazi, kutambua na uwajibikaji. Kuwapa wasikilizaji hali ya umiliki wa huduma za umma zinazotolewa.

Mfumo: Ujumbe wa maandishi, mahojiano na viongozi wa serikali za mitaa kutokana na ujumbe wa wasikilizaji.

Aina ya muingiliano: Ujumbe wa maandishi.

Maelezo: Trac FM (Shirika lisilo la kiserikali-NGO) linavipa vituo vya redio vifaa vya kupokea maoni katika mtandao. Wasikilizaji wanatuma ripoti au maoni juu ya mada zilizopendekezwa na mtangazaji, kwa lugha ya kiingereza au lugha ya kienyeji kwa ujumbe wa bure. Watangazaji wanapata matokeo ya papo kwa papo na ya wazi ya wasikilizaji, katika kompyuta zao za usimamizi ambazo wanawapatia tena wasikilizaji matokeo wakati wa kipindi hicho. Kituo kinawaalika viongozi wa serikali za mitaa kutoa maoni yao juu ya taarifa zilizokusanywa na Trac FM na kuhakikisha zinafika kwenye mamlaka husika.

Matokeo: Tathmini ya matokeo inaendelea. Trac FM inapendekeza kwamba makala hizo zinawapa sauti Waganda wa kawaida wasio na njia nyingine yoyote ya kutoa maoni yao.

Kwa taarifa zaidi: Sauti ya America, Februari 3, 2012. Kipindi kipya cha redio kinawapa Waganda sauti ya Umma. http://www.voanews.com/content/innovative-radio-talk-shows-give-ugandans-a-public-voice-138712619/159555.html
TRAC FM Tovuti at http://www.trac.pro/
TRAC FM Ikisimamia utoaji wa huduma. YouTube video at: http://www.youtube.com/watch?v=Lx_BivgFyww

8. Peace FM, Joy FM (Accra, Ghana)

Jina la programu: Wo haw ne sen (Akan language); Mwitiko (Kiingereza – haipo tena hewani)

Sababu za kuanzisha programu: Kutoa muda kwa wasikilizaji waeleze matatizo wanayokumbana nayo huko Accra. (huduma za binafsi auza umma) in Accra.

Mfumo: Simu, ujumbe, (Peace redio), na mahojiano na viongozi wa serikali za mitaa kutokana na maoni.

Aina ya muingiliano: Wasikilizaji wanapiga simu au kutuma ujumbe wa maandishi.

Maelezo: Wasikilizaji wanapiga simu au kutuma ujumbe wa maandishi wenye malalamiko juu ya huduma za umma au za binafsi. Vituo vinafuatilia malalamiko hayo na kujaribu kuhakikisha taasisi zinazohusika zinajibu au kutatua matatizo hayo inapohitajika. Vituo hivyo vinatangaza hewani iwapo tatizo hilo limetatuliwa au la. Mwitiko maofisa wahusika wanaalikwa kituoni kujibu maswali na kupokea miito ya simu za wananchi. Jopo la kudumu hapo kituoni akiwemo mwanasheria, daktari na mtaalamu wa masuala ya kompyuta. Jopo linatoa majibu na suluhisho miito inayohusu afya, sheria na mengine.

Matokeo: Mwitikio wa watangazaji wa redio kuhusiana na malalamiko hayo yanapangwa kwa ustadi mkubwa, kutokana na uchunguzi wa kina, na majibu ya maofisa kutoka kwa vyanzo vinavyohusika. Watangazaji wanayachunguza malalamiko hayo na kuthibitisha kuwa ni halisi. Kwa mfano, mtangazaji mmoja alipigiwa simu na mchuuzi wa mtaani kwamba watumishi wa Halmashauri ya mji walikuwa wakiwanyanyasa wachuuzi na wakiwaibia vyombo vyao kwa kisingizio kwamba walikuwa wanawaondoa viambazani. Kufuatilia, mtangazaji alijifanya kama mchuuzi na akaungana na wachuuzi wengine kiambazani hapo.

Ingawa hakufanyiwa vile Yule mchuuzi alivyofanyiwa lakini aliweza kupata ushahidi na akalipeleka suala hilo mbele kunakohusika.

Joy FM na Peace FM vilikuwa ni vituo vya redio vinavyosikilizwa na kuaminiwa sana mjini Accra. Kati ya wale waliokuwa wakiisikiliza Peace FM, karibia watu sita kati ya kumi walikuwa wasikilizaji wa Wo haw ne sen, Wakati nusu ya wasikilizaji wa Joy FM walisikiliza mwitiko huo uliporushwa hewani. Kwa mwitiko, asilimia 50-60 ya matatizo yaliyoibuliwa na wasikilizaji kati ya 2005-2008 yalitatuliwa, ikiwa na maana kwamba tatizo hilo lilichunguzwa na timu hiyo. Wakawasiliana na taasisi zinazohusika, na mwitiko wa mwishoni ukarushwa hewani kwamba tatizo hilo limeshatatuliwa.

Kwa maelezo zaidi: Edem E. Selormey, 2012. Rethinking citizen voice: Suala la miito mjini Accra, Ghana. http://www.institutions-africa.org/filestream/20120814-rethinking-citizen-voice-the-case-of-radio-call-ins-in-accra-ghana

Maswala mengine

Masuala ya kuwajibika na usalama kwa ajili ya programu za muingiliano.Ni muhimu sana wakati unapotangaza programu ya muingiliano kuzijua na kuzifuata sheria za nchi yako kuhusu kashfa, uzushi na kwa ujumla yale yanayokubalika katika utendaji wa uandishi wa habari. Jizoeze kuzifahamu sheria, kanuni na taratibu. Nchi nyingi zinakuwa na baraza la habari linalosimamia vyombo vya habari na kuviadhibu vituo vya redio na watu mbalimbali wanaovunja sheria, taratibu na miiko ya utendaji.

Baadhi ya serikali na watu binafsi au vikundi wanaweza pia kuwaadhibu (kwa hatua za kisheria juu ya masuala kama vurugu na/au vitisho) wale wanaotangaza masuala ambayo hawayapendi. Pamoja na kwamba watangazaji wanakuwa na haki ya uhuru wa kusema ndani ya sheria za nchi, ni muhimu sana kwa watangazaji kutumia akili na kujiweka katika mazingira ya usalama.

Taarifa Zaidi

DW Academie: Vidokezo 10 vya jinsi ya kuwa mwenyeji mzuri: http://blogs.dw-akademie.de/africa/?p=1313
DW Academie: Vox Pop: Mazuri na mabaya kuhusiana na mfumo huu wa uandishi. http://blogs.dw-akademie.de/asia/2012/05/18/vox-pop-whats-good-and-bad-about-this-journalistic-format/
PANOS Eastern Africa. Kuweka mambo sawa: Mwongozo kwa mwandishi kuendesha Mdahalo wa redio ya Jumuia. 2011.< a href="http://www.panosea.org/resources/publications/RRD%20Debate%20Guide%20full%20Doc%20A5.pdf"> http://www.panosea.org/resources/publications/RRD%20Debate%20Guide%20full%20Doc%20A5.pdf
http://radio.frontlinesms.com/2012/08/frontlinesmsradio-adds-an-exciting-tool-to-the-mix-at-rite-fm-ghana/

Acknowledgements

Umechangiwa na: Vijay Cuddeford, Mhariri mtendaji, Farm Radio International.
Imepitiwa na: David Mowbray, Meneja, Mafunzo na usanifu, Farm Radio International; Blythe McKay, Meneja, Kujengea uwezo watangazaji, Farm Radio International

Mradi huu umeandaliwa kwa msaada wa kifedha wa Serikali ya Kanada kupitia Wakala wa kimataifa wa Maendeleo wa Kanada (CIDA)