Njia za kujifunza na kujua ni nini wasikilizaji wa kipindi chako wanahitaji

Maelezo/Vidokezo kwa Mtangazaji

Kipindi cha redio kinaweza kukidhi matakwa ya wasikilizaji zaidi kama kutakuwa na njia za kupata mrejesho ya nyuma kutoka kwao.

Ili uweze kutengeneza kipindi cha redio cha kilimo chenye kukidhi mahitaji ya wasikilizaji unapaswa kuzingatia mambo yafuatayo:
1) Jitahidi kufahamu wasikilizaji wako.
2) Famahu taarifa/habari za kilimo zenye umuhimu kwao.
3) Famamu namna ya kuwashirikisha wakulima ipasavyo kwenye majadiliano ya redio juu ya mambo muhumi wanayoyaona.

Ni lini redio yako ilifanya tathimini/utafiti kiundani ili kufahamu hali anayokumbana nayo mkulima/wasikilizaji wako kwa mara ya mwisho? Huenda ikakupasa kurudia tena utafiti/tathmini hiyo sasa!

Maelezo haya ni kwa ajili ya kukupa mwongozo juu wa ushirikishaji wa jamii ya wasikilizaji katika vipindi vya redio ipasavyo, ili kukidhi mahitaji yao vizuri zaidi. Maelezo haya yamegawanywa katika sehemu kuu mbili: Sehemu ya kwanza inaelezea mambo unayoweza kufanya ili kujifunza mahitaji ya hadhira/wasikilizaji wako, mambo ambayo wangependa kuyasikia. Sehemu ya pili ina maswali ambayo yatakusaidia kufasili/kufafanua aina ya hadhira/wasikilizaji unaowalenga.

Sehemu ya 1: Ni taarifa/habari gani msikilizaji/mkulima angehitaji kupata?

Utangulizi

Ni chanzo gani cha habari/taarifa kilicho muhimu kupita vyanzo vyote, kinachoweza kukupatia taarifa zinazohitajika na hadhira ya wakulima wasikilizaji? Hakika ni wakulima ambao ndio hadhira yako!

Ingawaje njia nyingine za kitafiti zimetajwa kwenye maelezo haya, inapendekezwa uwatembelee wakulima/wasikilizaji katika mazingira ya jamii zao. Safiri kwenda vijijini, fanya mikutano na makundi mbalimbali ya wakulima. Kama wakulima wanawake wanaona aibu kuongea mbele ya wanaume, basi watenganishe na wanaume kwa kufanya mikutano ya wanawake peke yao na wanaume peke yao.

Baadhi ya vituo vingine vya redio vinaweza kutumia muda mwingi vijijini vikifanya mazungumzo na wakulima, kurekodi sauti zao, na kufanya mikutano ambayo inawapa wakulima fursa ya kuzungumzia juu ya aina ya taarifa wanazohitaji zaidi.

Kuna sababu nyingi zinafanya vituo vingine vya redio kushindwa kuwatembelea wasikilizaji vijijini. Lakini bila kujalisha kituo chako ni muhimu kufanya majadiliano na wasikilizaji wako kadiri inavyowezekana.

Kulingana na rasilimali ulizonazo kiwango cha mahusiano yako ya nyuma na jamii ya wasikilizaji wako, pamoja na uzoefu wako na mafunzo ya utafiti wa wasikilizaji, kuna mambo kadhaa ya kitafiti unaweza kufanya unapoitembelea jamii ya wasikilizaji wako. Yote hayo yatahusisha mazungumzo na wakulima kwa hiyo kukumbuka kwamba kujenga uhusiano ni kiungo muhimu sana katika uandaaji wa vipindi bora na shirikishi.

Kwa vituo vyenye hali ya uhaba wa rasilimali au elimu ndogo ya utafiti wa wasikilizaji au mawasiliano madogo na jamii, huenda wangependa kujaribu kutumia Shughuli Tano za Kitafiti zilizoorodheshwa hapo chini:

Kama kituo chako kimekuwa na mawasiliano duni na jamii ya wasikilizaji, ni vyema ukaanza kukutana na wasikilizaji wako kwa njia isiyo rasmi, kama vile “kukutana nao chini ya mwembe.” Katika mazingira yasiyo rasmi, unaweza kuuliza swali moja au maswali machache mapana zaidi na kuwaruhusu wasikilizaji wako kuongea kwa uhuru wakati wakijibu maswali hayo. Kwa mfano, ungeweza kuwauliza ni jinsi gani kituo chako kingeweza kuboresha huduma zake ili kuwahudumia wakulima kwa ufanisi zaidi. Unaweza pia kuwauliza ni habari gani za kilimo ni muhimu zaidi kwao.

Mbinu hii ya kuuliza maswali machache na mapana inaweza kuwaruhusu wasikilizaji kushiriki kwa uhuru zaidi katika kuamua maudhui au kuweka agenda kwa ajili kipindi chako cha Farm Radio. Kama unahitaji kupata maoni/mrejesho nyuma juu ya masuala ya kilimo, hakikisha kuwa maswali yanayohusu kilimo yanakuwa mapana iwezekanayo, labda unaweza kuyapanua yakagusa nyanja zote za maisha (Maisha ya wakulima yanahusu njia zote zinazowatengenezea kipato).

Kwa vile vituo vya redio vyenye rasilimali zaidi na mafunzo, na vyenye mawasiliano ya mara kwa mara na jamii ya wasikilizaji wao wanashauriwa kujaribu kutumia Shughuli Tatu za Ziada za Utafiti zitakazotajwa hapo baadaye katika mtiririko huu wa maelezo. Lakini bila shaka uko huru kujaribu shughuli yoyote kama ilivyoelezwa.

Huenda baadhi ya shughuli zilizoorodheshwa hapa chini zikawa ni mpya kwako. Tunakuhimiza ujaribu kufanya kitu ambacho hujawahi kufanya. Hata hivyo inaweza ikawa nzuri zaidi kama utawauliza wakulima kama wangependa kukuona ukijaribu kitu kipya ili muweze kujifunza kwa pamoja. Huenda wakakukubali na kufurahi kwa kuwa umewaomba ruhusa, kwa hiyo unapaswa kuwa na subira zaidi kwenye mchakato mzima.

Umuhimu wa kuwa na Fikra/Mawazo sahihi ya Kitafiti

Unapokutana na wakulima kwa lengo lolote liwalo, kila mara unapaswa kukumbuka kwamba unakutana nao ili uweze kujifunza kutoka kwao. Usihofu kwamba unatakiwa kukamilisha kila kitu kwenye ziara ya mara ya kwanza. Unapaswa kuchukua hatua kwa kujenga mahusiano ya muda mrefu yanayohusisha pande mbili ambayo ni kituo chako na wakulima, Ili kujenga mahusiano mazuri na ya muda mrefu. Heshima na utulivu ni muhimu sana, kuwa mnyenyekevu, mwenye heshima, na mvumilivu wa kutaka kusikiliza mambo ambayo wanakijiji wangependa kusema na kukuonyesha. Kuwa mtulivu usiwe na papara. Kuwa mtulivu sikiliza kwa makini, tizama na usingilie maongezi, kwa kufanya hivyo utaweza kujenga mahusiano zaidi na wanakijiji.

Kuheshimu kazi wanazofanya wakulima pamoja na mawazo yao, kunaweza kuwafanya wakulima wawe tayari kukukaribisha kwa mara nyingine kwenye jamii zao. Ni muhimu pia kuwa mwaminifu na muwazi tangu mwanzo. Waeleze kwamba madhumuni ya ziara yako ni kukutana nao na kupata mchango wao wa kimawazo. Na kwamba mawazo yao yatakusaidia katika kubuni vipindi vya redio ambavyo vitawasaidia katika shughuli zao za kilimo.

Shughuli Tano za Kitafiti

Hizi ni njia rahisi kiasi zitakazokusaidia kuwasiliana na jamii ya wasikilizaji na kujua aina ya taarifa za kilimo wanazohitaji:

Matumizi ya Vipindi vya redio na Simu za Mkononi Kukusanya Taarifa za vipindi vya redio

Kama una kikundi cha wakulima kilicho hai, tengeneza shoo itakayowaruhusu kupiga simu na kujadili masuala ya kilimo ambayo ni muhimu zaidi kwao.

Ujumbe wa Simu Uliorekodiwa (sauti pepe).
Tengeneza mfumo wa kurekodi sauti na uwaambie wakulima na uwapige simu na kutaja njia kuu za kilimo na maswala ya usalama wa chakula.

Ujumbe Mfupi wa Simu (SMS).
Kuna njia kuu mbili za kutumia SMS. Kwanza, unaweza kuomba kupata maoni juu ya maswali maalum. Wenyeji wako wa uendeshaji wa kipindi watauliza maswali na kuwaomba wakulima wayajibu kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu – SMS. Unaweza kuuliza maswali tofauti kwa siku tofauti au kutengeneza maswali ya kuchagua ili wasikilizaji waweze kujibu swali fulani. Kwa mfano, unaweza kuuliza swali ambalo wasikilizaji wanaweza kujibu ndiyo au hapana, AU daima, wakati mwingine, mara chache, au kamwe. Tengeneza jedwali linaloonyesha idadi ya kura zilizopigwa na wakulima kwa kila orodha ya majibu waliyotakiwa kuchagua kwa mfano, ni wangapi wamejibu ndio na wangapi hapana, fanya hivi kwa maswali yote. Kama unaweza kutumia huduma kama vile FrontlineSMS, unaweza kukusanya meseji zote kwenye kompyuta. Bila shaka umuhimu wa matumizi ya ujumbe wa maandishi unategemeana na upatikanaji wa simu za mkononi na uwezo kusoma na kuandika wa watumiaji. Kujibu swali kwa kutumia meseji kunaweza kusitoe sampuli sahihi inayoweza kuwawakilisha wakulima katika jamii.

Pili unaweza kuuliza maswali mapana kuhusu kilimo au maisha kwa ujumla au kuwajulisha wasikilizaji wako kuwa kituo chako kingependa wasikilizaji waseme ni aina gani ya kilimo na masuala ya usalama wa chakula ni muhimu zaidi kwao. Hatulengi njia hii sana lakini kama umekuwa na mahusiano madogo na jamii ya wasikilizaji wako, njia hii inaweza kuwa bora katika kuwahamasisha kuwaeleza mahitaji yao muhimu zaidi.

Ziara ya masoko ya kijamii.

Masoko ya jamii ni sehemu nzuri ya kukutana na wakulima, na mara nyingi wakulima hawa hutoka kwenye jamii mbalimbali, Inawezekana ukashindwa kufanya mikutano au majadiliano na vikundi lakini mkulima mmoja mmoja anayeuza bidhaa sokoni anaweza kukupa picha nzuri juu ya nguvu na madhaifu ya wakulima katika jamii hiyo na fursa na changamoto zinazowakabili.

Ongea na mashirika ya kilimo.

Kama kuna mashirika ya kilimo ya kijamii au vyama vya ushirika vinavyoweza kuitisha mikutano ya mara kwa mara, unaweza kukutana nao na kupata taarifa muhimu kuhusu masuala muhimu ya kilimo katika jamii hiyo.

Majadiliano na watoa huduma za ugani za kilimo.

Kulingana na uwezo wa huduma za ugani katika jamii husika, hii inaweza kuwa ni njia nzuri ya kujifunza juu ya mahitaji ya mkulima. Baadhi ya maofisa wa ugani wanaweza kuwa na ufahamu mzuri wa mahitaji halisi ya wakulima wakati wengine wanaweza tu kuorodhesha vipaumbele vya wizara ya kilimo, vipaumbele ambavyo vinaweza kuwa tofauti kabisa na vile vya wakulima wadogo. Hebu chukulia kama unaongea na maafisa ugani wa serikali na wale wanaofanya kazi katika mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), mashirika ya wakulima na huduma binafsi.

Fanya Ziara Mashambani.

Pamoja na wajumbe wa timu yako tembeleeni kijiji kimoja au viwili vya kawaida katika eneo la wasikilizaji wenu. Jaribuni kuchagua vijiji ambavyo matatizo ya kilimo ni kawaida. Kabla ya kufanya ziara yenu mnapaswa kufahamu taratibu za jamii husika na kuzizingatia wakati wa uendeshaji wa mikutano yenu. Kwa mfano, hili linaweza kutumika kwenye mkutano na viongozi wa kijamii, au kuomba kibali cha mkutano kutoka kwa mamlaka hizo. Kuzingatia na kufuata desturi hizi kwa umakini kutawafanya mheshimike katika jamii na kurahisisha kazi yenu.

Hizi ni baadhi ya dondoo kwa ajili ya mikutano na jamii:

  • Mkutano usio rasmi "mkutano wa chini ya mwembe"
  • Kurekodi majadiliano ya wanakijiji kwa mara moja kwa mwaka, mara tatu kwa mwaka, kila mwezi, au mara kwa mara zaidi
  • Kikao kwenye "ukumbi wa mji" Mkutano na kiongozi wa jadi (aina hii ya mikutano hujulikana kwa majina tofauti katika nchi na tamaduni mbalimbali).

Mikutano hii inaweza kuwa na agenda pana kabla ya kuitishwa kwa mfano, wanakijiji wanaweza kutaka kuzungumzia juu ya mahitaji yao muhimu ya kilimo, matatizo yao muhimu ya kimaisha, aina ya taarifa ambazo wangependa kusikia kwenye vipindi vya redio, changamoto kuu wanazokutana nazo kwenye kilimo au jinsi kituo cha redio kinaweza kuboresha huduma za kijamii. Unapowasiliana na jamii ili kufanya maandalizi ya mkutano unapaswa kujadiliana nao kuhusu lengo la mkutano litakuwa nini.

Kwa kawaida wanasayansi ya jamii huandaa dodoso lenye maswali ya kuchagua kwa ajili ya kukusanyia taarifa. Mnashauriwa kujaribu njia hii hasa kama mnafahamika katika jamii husika na kama mna mafunzo kiasi juu ya aina hii ya utafiti. Kwa mwongozo zaidi soma Shughuli Tatu za Ziada za kitafiti zinazotumia muundo maalum zaidi.

Bila kujali umetumia dodoso au kuuliza maswali mapana ni muhimu kuchambua mazungumzo yako kwa kuzingatia suala la uwezo, udhaifu, fursa na changamoto zilizoibuka. Mbinu zitumiazo muundo dodoso mara nyingi hutumia maswali mahususi kufahamu uwezo , udhaifu, fursa na changamoto au vikwazo. Muundo wa maswali haya ni mahususi kwa kukusanya taarifa juu ya mambo yafuatayo:

Uwezo wa wakulima kutoa mchango kwa ajili ya mafanikio yao katika kilimo, Kwa mfano:

  • Zao za kilimo.
  • Ujuzi wao wa udongo, mbegu na mazao.
  • Ujuzi wao wa kilimo.
  • Masoko ya mazao yao.
  • Zana za kilimo wanazomiliki.
  • Upatikanaji wa watenda kazi (labda watoto wao wakubwa na ndugu wengine).

Udhaifu unaowafanya wakulima wasiweze kutumia uwezo wao wote katika kutimiza malengo yao kwa mfano:

  • Ugumu wa upatikanaji wa ardhi, mbegu, maji na pembejeo nyingine.
  • Ukosefu wa ujuzi wa kilimo unaomwezesha mkulima kulima kwa ufanisi zaidi.
  • Ukosefu wa masoko ya mazao yao.
  • Ukosefu wa watenda kazi wa kutosha wakati wa msimu wa kilimo.
  • Udongo usio na rutuba, mbegu zenye viwango duni, au mazao yenye kushambuliwa na magonjwa na wadudu kirahisi.
  • Ukame, ongezeko la wadudu waharibifu, na misimu ya mvua isiyotabirika.
  • Matatizo ya kiafya, majeraha, au hali nyingine zinazowazuia wakulima kufanya kazi.

Fursa zinazoweza kuwafanya wakulima wanawake kwa wanaume waboreshe maisha yao kwa mfano:

  • Aina mpya ya mazao sokoni.
  • Njia mpya za kuongeza rutuba kwenye udongo na uzalishaji wa mazao.
  • Njia mpya za kuhifadhi mazao na kuyalinda.

Changamoto au hatari zinazowakumba wakulima kwa mfano:

  • Mabadiliko ya tabia nchi.
  • Machafuko ya kisiasa.
  • Kushuka kwa bei au mahitaji ya soko.
  • Uhaba wa pembejeo kama vile mbegu au mbolea.

Utaweza kutumia taarifa utakazopata kwenye ziara vijijini katika kufanya maboresho kipindi cha mkulima.

Ziara ya shambani
Wakati ukiwa kwenye jamii, unaweza kumtembelea mkulima na kumwomba akuonyeshe shamba lake. Ni wazo zuri kupanga ziara hii kabla ya kukutana na jamii muulize mkulima kuhusu kalenda ya kilimo ni mazao yapi analima katika nyakati tofauti za mwaka. Uliza maswali kuhusu unatakachokiona na kuhusu jinsi mkulima anavyoendesha shughuli zake au mabadiliko ambayo mkulima anatarajia kufanya siku zijazo.

Shughuli tatu za ziada za utafiti.

Kwa wale wenye uzoefu zaidi au mafunzo zaidi katika utafiti wa wasikilizaji na wenye mahusiano ya karibu zaidi na jamii, haya hapa ni mazoezi matatu ya ziada yenye muundo maalumu ambayo unaweza kufanya wakati wa ziara zako vijijini ili uweze kukusanya taarifa:

1)Kukusanya kundi la wakulima kwa ajili ya "lengo la majadiliano kwenye kundi"

Lengo la majadiliano ya vikundi ni lipi? Kwa kifupi hiki ni kikundi cha watu kinachoongozwa na mwezeshaji kuzungumza kwa uhuru kuhusu masuala maalum. Majadiliano ya vikundi kwa mara nyingi huhitaji watu kujibu maswali maalum, ingawaje maswali hayo yanaweza kuwa mapana sana au mafupi na mahususi zaidi.

Jiwekee lengo la kuwa na angalau majadiliano na kikundi kimoja cha wakulima wa kike, mengine na kikundi kimoja cha wakulima kiume na kama ikiwezekana fanya majadiliano pia na kikundi kimoja cha wakulima vijana, unaweza pia kuwa na majadiliano na wakulima wazee. Fanya maandalizi kwa ajili ya majadiliano hayo kwa kubuni baadhi ya maswali muhimu. Baada ya kila swali muhimu uliza maswali ya ziada kulingana na jinsi washiriki watajavyokujibu. Hakikisha kwamba kila mshiriki katika kikundi anapata fursa kuchangia, Muombe mmoja wa wajumbe wa timu yako achukue maelezo ya kina na kurekodi sauti ya majadiliano hayo ili wewe uweze kujihusisha zaidi katika kuuliza maswali mazuri na kusikiliza majibu yao kwa umakini zaidi.

Haya ni baadhi ya maswali ya mfano ambayo yanaweza kukusaidia katika kuanza na kuongoza majadiliano yako, Kumbuka kwamba ni muhimu kujua ni kwa nini wakulima wametoa majibu waliyokupa tumia mbinu hii, epuka matumizi ya neno “kwanini” wakati unapowezesha mjadala ni jukumu lako kujua ni kwanini. Kwani kutakusaidia kuelewa hali halisi waliyo nayo.

Swali (Kuhusu uwezo)
Je, ni nini kinakwenda vizuri katika shughuli zako za kilimo kwa sasa? Tafadhali elezea jinsi shughuli zako za kilimo zinavyokwenda vizuri au Tafadhali toa maelezo ya kina zaidi au Tafadhali elezea, (maswali haya yanamtaka mkulima atoe maelezo ya undanii zaidi na yanaweza kutumika katika kubaini uwezo, udhaifu, fursa, au changamoto).

Kulingana na majibu utakayopata, maswali ya kufuatilia yanaweza kuhusisha yafuatayo:

  • Ni mazao yapi/mifugo ipi inakuleta mafanikio zaidi?
  • Wewe kama mkulima, ni nini unamudu zaidi katika shughuli zako za kilimo?
  • Unamiliki zana au pembejeo gani zinazokusaidia katika kilimo?
  • Ni nani/kina nani wanakusaidia katika shughuli zako za kilimo?

Swali (kuhusu udhaifu): Je, ni nini hakikuendei sawa katika shughuli zako za kilimo kwa sasa? Tafadhali fafanua

Maswali ya ziada yanaweza kuwa ni pamoja na:

  • Ni mazao gani/mifugo ipi inakuletea shida? Ni kwa jinsi gani?
  • Ni aina gani ya pembejeo hazipatikani kirahisi?
  • Je, kuna taarifa au maarifa yotote muhimu usiyokuwa nayo?

Swali (kuhusu fursa): Je, kuna mambo unadhani yanaweza kutokea siku za usoni yanayoweza kukusaidia katika shughuli zako za kilimo? Tafadhali fafanua

Maswali ya ziada yanaweza kuhusisha yafuatayo:

  • Je, kuna huduma zozote za kiserikali/ruzuku/sera ambazo zinaweza kukusaidia?
  • Je, kuna miradi yoyote mipya ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) ambayo inaweza kukusaidia?
  • Je, kuna fursa yoyote mpya ya masoko ambayo inaweza kukusaidia?

Swali (kuhusu changamoto au vitisho): Je, kuna jambo lolote linaloweza kutokea katika siku zijazo linaloweza kuathiri shughuli zako za kilimo?

Kulingana na majibu, maswali ya ziada yanaweza kuhusisha yafuatayo:

  • Je, una wasiwasi wa kunyang’anywa shamba siku zijazo?
  • Je, una hofu juu ya mabadiliko ya tabia nchi?

Ni muhimu pia kufahamu nafasi ya wakulima kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya biashara. “Mnyororo wa thamani” katika kilimo unaweza kutafsiriwa kama: shughuli zinazofanyika katika kuleta bidhaa za kilimo kama vile mahindi au mboga au pamba kutoka kwenye maeneo ya uzalishaji mpaka kuwafikia walaji, kwa kupitia ngazi mbalimbali kama vile usindikaji, ufungaji, na usambazaji.

Swali (kuhusu mnyororo wa thamani): Waulize wakulima kama wanauza mazao yao yote au sehemu ndogo tu.

Maswali ya ziada ni pamoja na:

  • Je, wanauzia wapi mazao yao? Kwa nani?
  • Je, wamejiunga na vyama vya ushirika?
  • Je, wanaridhika na bei wanazopata?
  • Je, wanasindika aina ya mazao wanayozalisha? Kupitia vyama vipi vya ushirika?
  • Je, ni wao au vyama vyao vya ushirika vinauza bidhaa za mazao yao yaliyosindikwa? Je, zinauzwa rejareja? Je, zinauzwa kwa jumla kwa wazalishaji wa bidhaa nyingine?
  • Je, vipi kuhusu pembejeo? Wananunua wapi pembejeo? Je, wanaridhishwa na bei ya wanazotozwa kwa ajili ya pembejeo?
  • Je, wanaridhika na nafasi zao katika mnyororo wa thamani? Je, wanahisi kuwa wanatendewa haki?

Kwa maelekezo zaidi kuhusu jinsi ya kufanya majadiliano kwenye vikundi tafadhali soma kipengele cha 3 kwenye Farm Radio Resource Pack.

2)Maongezi wakati wa kutembea

Haya ni mazungumzo kati yako na wakulima kadhaa vijijini ambayo hufanyika wakati unatembea kutoka upande mmoja hadi mwingine katika kijiji. Waombe wanakijiji wachague njia itakayokusaidia kuona utofauti zaidi katika suala la mazingira na kilimo. Kazi yako ni kuchunguza, kusikiliza, na kuuliza maswali kuhusu unachoona katika maeneo utakayopita.

Waombe wakulima wakutajie kitu chochote wanachopenda, ikiwa ni pamoja na:

  • Aina ya mazao wanayolima au mifugo wanayofuga.
  • Hali ya mazingira inavyowasaidia au kuwapa changamoto zaidi katika kilimo (kwa mfano, milima inaweza kuongeza mmomonyoko wa udongo, na mto unavyoweza kutumika kwa ajili ya umwagiliaji).
  • Maeneo ya jumuiya na ya hifadhi.

Hakikisha unauliza maswali mengi iwezekanavyo kwa mfano, unaweza kuwauliza:

  • Kama wanaume/wanawake wanalima aina fulani ya mazao.
  • Ni nani mwenye haki ya kumiliki ardhi.
  • Ni kina nani katika familia wanafanya maamuzi yahusuyo kilimo.
  • Ni nani anamiliki rasilimali (wanaume au wanawake, vijana, wazee au wenye umri wa makamo, tamaduni zipi au makundi ya kikabilia, maskini au matajiri).
  • Mzunguko wa mazao unazingatiwaje.

Hakikisha kuna mtu anayekusaidia kuandika mnayoona na kujadili.

3) Zoezi la kuandaa orodha

Omba kikundi cha wakulima 8-10 kikusaidie kutengeneza orodha ya aina ya taarifa ambazo wanadhani zingeweza kuwasaidia katia shughuli zao za kilimo. Orodha hii inaweza kuhusu mambo yafuatayo:

  • Bei katika masoko ya ndani na ya kikanda.
  • Utabiri wa hali ya hewa wa nchi husika.
  • Taarifa kuhusu mbegu.
  • Taarifa kuhusu uboreshaji wa rutuba ya udongo.
  • Taarifa kuhusu usindikaji na uhifadhi wa mazao baada ya kuvuna.
  • Taarifa kuhusu masoko wanayopendelea zaidi.

Jaribu kugawa orodha hiyo katika aina 4-6 za taarifa. Kisha waombe wanakikundi wafanye kazi ya kuonyesha kwa kuorodhesha na kuanza na jambo ambalo ni muhimu kuliko yote na kumalizia na lile lenye umuhimu mdogo kuliko yote. Kwa kushirikiana na wakulima chagueni vitu vitakavyowakilisha aina tofauti za taarifa. Kisha wape wakulima mawe 20 na waombe waamue kwa pamoja aina gani ya taarifa ni muhimu kuliko zote na ni ipi ina umuhi mdogo kuliko zote. Wanaweza kufanya hivyo kwa kuweka mawe mengi zaidi karibu na aina ya taarifa ambazo wanadhani ni muhimu na mawe machache zaidi karibu aina nyingine za taarifa.

Wape wanakikundi muda wa kutosha kufanya maamuzi. Wakulima wanaweza kuweka mawe sehemu moja ya aina ya habari na kuyarudisha sehemu nyingine baadaye, kabla ya kufikia muafaka. Jitahidi kusikiliza kwa makini, na kuandika maelezo ya majadiliano wanayofanya wakati wakiwa katika mchakato wa kuafikiana juu ya aina ya habari ambayo wanadhani ni muhimu zaidi. Kwa kusikiliza, utaweza kujifunza ni kwa nini aina moja ya habari ni muhimu zaidi kuliko nyingine.

Jedwali lililopo hapo chini ni la mfano unaoonyesha jinsi wakulima wanaweza kuonyesha umuhimu wa aina nne tofauti ya taarifa.

Sehemu ya II: Kujua wasikilizaji wako.

Sehemu ya pili ya maelezo haya inatoa baadhi ya mawazo juu namna ya kujua sifa – ukubwa wa mashamba, ukubwa wa familia, mazao makuu na mifugo, kusikiliza vipaumbele vya wasikilizaji wako.

Taarifa hii itakusaidia kuwafahamu wasikilizaji wako. Hii inaweza kuwa ni hadhira unayolenga kwa ajili ya kipindi cha kilimo: wakulima wa kiume, wakulima wa kike, wakulima wa kahawa, wakulima wadogo wadogo, wakulima watumiao kilimo hai, wakulima wenye umri mdogo, wakulima wa kibiashara, vijana wenye umri kati ya miaka 14-25, wanafunzi wa shule za sekondari, watu wenye elimu msingi. Unaweza kutengeneza orodha kubwa sana ya hadhira.

Ili kipindi chako kiweze kuwavutia wasikilizaji itategemeana na aina ya jamii unazolenga na aina mbalimbali ya kilimo zinazotekelezwa katika eneo linalofikiwa na kituo chako cha redio. Unaweza kujaribu kuchunguza hili jambo wakati wa ziara yako na utakapokuwa unajadiliana na jamii ya wasikilizaji wako.
Makundi mawili ya maswali hapo chini yatakusaidia katika kufafanua aina ya wasikilizaji wako. Inaweza ikawa vigumu kupata majibu sahihi ya maswali haya, na huenda ikawa vigumu kupata takwimu sahihi. Hivyo basi unatakiwa kutafuta taarifa zako na kufanya makadirio mazuri wewe mwenyewe.

Inawezekana usipate taarifa kuhusu maswali yote yaliotajwa. Usijali; kinachojalisha zaidi ni kufikiria kuhusu maswali kama haya na kujaribu kuyapatia majibu mengi na yenye maana kadri iwezekanavyo.

Taarifa kuhusu idadi ya watu (taarifa kuhusu watu na wanachokifanya):

  • Uwiano ukoje (kwa mfano, moja ya robo, nusu, robo tatu, asilimia 95%) juu ya watu wazima katika eneo unalolenga kurusha kipindi chako; kutegemea kwao kilimo au ufugaji kama sehemu tu au tegemeo kubwa katika maisha?
  • Shamba lina ukubwa wa wastani gani?
  • Familia inayotegemea kilimo ina watu wangapi?
  • Uwiano wa wakulima wadogo ukoje?
  • Uwiano wa wakulima wakubwa au wakulima wa bidhaa za kibiashara ukoje?
  • Wastani wa kipato kwa familia za wakulima ukoje?
  • Je, kuna msimu mbaya au wa njaa katika eneo husika? Kama ndiyo, ni wakati gani?
  • Je wakulima wanakabilianaje na hali ya njaa?
  • Je, familia za wakulima zinapata huduma nzuri za kilimo?
  • Je, uwiano wa familia za wakulima wadogo vijijini sizizo na uwezo wa kuuza kitu chochote katika masoko ukoje?
  • Uwiano wa familia zinazotegemea masoko kwa ajili ya kipato ukoje?
  • Uwiano wa familia za vijijini zenye vyanzo vingine vya mapato, mbali na shughuli za kilimo ukoje?
  • Ni aina ipi kuu ya mazao na mifugo ipo katika eneo husika?
  • Ni nini wakulima wa kike hufanya tofauti na wakulima wa kiume?
  • Uwiano wa vijana wanaojihusisha shughuli za kilimo ukoje?
  • Uwiano wa wanaume vijijini wanaojua kusoma na kuandika ukoje?
  • Uwiano wa wanawake vijijini wanaojua kusoma na kuandika ukoje?

Maswali yanayohusuyu upatikanaji wa redio.

  • Ni uwiano gani wa wakulima wa kiume (kwa mfano, moja ya robo, nusu, robo tatu, asilimia 95%) wanaweza kusikiliza vipindi vya redio nyumbani kwao?
  • Ni uwiano gani wa wakulima kike wanaweza kusikiliza vipindi vya redio nyumbani kwao?
  • Je, redio yako inafikisha mawasiliano vizuri kwenye eneo lote unalorusha matangazo?
  • Ni uwiano gani wa wakulima wa kiume wanasikiliza vipindi vya redio katika vikundi?
  • i uwiano gani wa wakulima wa kike wanasikiliza vipindi vya redio katika vikundi?
  • Wakulima wa kiume wanapenda kusikiliza vipindi vipi vya redio?
  • Wakulima wa kike wanapenda kusikiliza vipindi vipi vya redio?
  • Wakulima vijana wanapenda kusikiliza vipindi vipi vya redio?
  • Wakulima wazee wanapenda kusikiliza vipindi vipi vya redio?
  • Fafanua/elezea ni kwanini vipindi hivyo ni muhimu?
  • Je, wakulima wa kiume wanapata taarifa za kilimo kutoka kwenye redio? Kama ni ndiyo, wanazipata kutoka vituo vipi vya redio na vipindi gani?
  • Je, wakulima wa kike wanapata taarifa za kilimo kutoka kwenye redio? Kama ndiyo, ni vituo vipi vya redio na ni vipindi gani?
  • Ni wakati gani wana familia hupendelea kusikiliza redio ili kupata taarifa za kilimo?
  • Ni wakati gani wakulima wa kiume hupendelea kusikiliza redio ili kupata taarifa za kilimo?
  • Ni wakati gani wakulima wa kike hupendelea kusikiliza redio ili kupata taarifa za kilimo?

Unaweza kufikiria maswali mengi zaidi kama haya. Majibu ya maswali haya yatakukusaidia kufahamu wasikilizaji wako walengwa.

Kumbuka kuwa unapaswa kuwa na lengo mahususi wakati unapojaribu kufahamu wasikilizaji wako. Huenda wasikilizaji unao walenga wasiwe “wakulima wote, wanaume kwa wanawake, wenye umri kati ya miaka 10 hadi 80, wenye shamba lenye ukubwa wa nusu hekari hadi hekari 100.” Mahitaji na aina ya kilimo kilichozoeleka na tofauti katika kikundi itakuwa kubwa sana pia, pia kutakuwa na tofauti katika aina ya vipindi watakavyopendelea. Hata hivyo, wakulima wadogo wadogo wengi katika eneo fulani wanaweza kuwa na masuala muhimu yanayofanana. Kipindi chako kinapaswa kutumia muda mwingi katika kujadili masuala haya yanayofanana, wakati huohuo unaweza kuendelea kuandaa vipindi vitakavyozungumzia mada zitakazoweza kutumiwa na sehemu ndogo ya wakulima kwenye jamii.

Inaweza kwamba wanawake hupendelea kusikiliza vipindi vya kilimo wakati wa kupika chakula cha jioni kwa sababu wakati huo wanaweza kuwa huru zaidi kusikiliza redio, mara nyingi huu ni wakati ambao waume zao wanakuwa na mapumziko mbali na nyumbani kwao. Kama ni hivyo, si wazo zuri kuendesha kipindi kinacholenga makundi yote mawili, labda kama itawezekana kuwa na marudio ili kuliwezesha kundi ambalo halitakuwa limepata fursa ya kukisikiliza waipate.

Hitimisho

Kumbuka kwamba utafiti wa wasikilizaji ni zoezi endelevu. Wasikilizaji wako wanabadilika baada mara kwa mara, hali kadhalika mahitaji yao kuhusu aina ya taarifa. Hivyo basi, ni muhimu kutengeneza mazingira ya heshima na ushirikiano. Unapaswa kutambua kwamba si wewe peke yako unatafuta taarifa kutoka kwenye jamii. Kumbuka kwamba kazi yako ni kuitumikia jamii ya wasikilizaji wako!

Shukrani

Imechangiwa na: Vijay Cuddeford, Mhariri Mtendaji, Farm Radio International, kutokana na nyaraka za Doug Ward, Mwenyekiti, Farm Radio International, Blythe McKay, Meneja, Rasilimali kwa Watangazaji, Farm Radio International, na David Mowbray, Meneja, Mafunzo na Rasilimali kwa ajili ya watangazaji, Farm Radio International.
Imepitiwa upya na: Doug Ward, Mwenyekiti, Farm Radio International

Mradi huu ulifanywa kutokana na msaada wa kifedha kutoka Serikali ya Canada kupitia Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo (CIDA)

For further information
Search for Common Ground, undated. Target Audiences for Peacebuilding Radio: A Training Guide. http://radiopeaceafrica.org/assets/texts/pdf/201010TargetAudience_EN_color.pdf
Graham Mytton, 1999. Handbook on Radio and Television Audience Research. http://www.cba.org.uk/wp-content/uploads/2012/04/audience_research.pdf
Sol Plaatje Institute for Media Leadership, 2009. Formative Target Audience Research: A Case Study of Five Community Radio Stations in South Africa. http://spi.ru.ac.za/images/stories/PDFs/publications/Formative_Target_Audience_Research.pdf